Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Serikali ya Romania imetoa ufadhili wa masomo ya udaktari na ufamasia kwa vijana 10 wa Kitanzania kwenda kusoma nchini humo, huku Tanzania ikitoa nafasi tano kwa vijana wa nchi hiyo kuja kusoma kozi yoyote hapa nchini.
Hayo amesemwa leo Novemba 17,2023, Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara ya Kitaifa ya Rais wa Romania, Klaus Lohannis nchini Tanzania.
Rais wa Romania, Lohannis yupo nchini kwa ziara ya siku tatu, kesho anatarajiwa kufanya ziara visiwani Zanzibar na atafanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Rais Samia amesema Serikali za Tanzania na Romania zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali nchini kama vile elimu, afya, kilimo, uwekezaji na kukabiliana na maafa ya majanga.
“Katika mazungumzo yetu na Rais Klaus yalijikita kwenye masuala mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, ufadhili wa masomo ya udaktari na famasia, kutoa nafasi 10 kwa ajili ya watanzania nchini Romania na nafasi tano kwa ajili ya kusoma Tanzania fani yeyote, “amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa kitu kingine wamekubaliana kuwepo na kiwanda cha kutengeneza dawa nchini , kusindika mazao na kujengeana uwezo katika utafiti wa kilimo, usalama wa chakula na maafa.
Kuhusu sekta ya biashara na uwekezaji, amesema itawakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Romania kwa pamoja kujadili fursa mbalimbali zinapatikana katika nchi hizo mbili.
Amesema uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulianza tangu mwaka 1964 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema ziara hiyo ya Rais Lohannis ni muhimu nchini ikizingatiwa ni kwa mara ya kwanza kufika nchini, hii ni kuonesha jinsi gani zinaendelea kuimarisha uhusiano wao.
Aidha Rais Samia amesema mwaka 2018 walisaini mkataba wa mazungumzo ya siasa lakini hawakutekeleza kutokana na ugonjwa wa UVIKO 2019, hivyo wamekubaliana wanatarajia kuanza mkutano wa kwanza mwakani kukuza ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Rais wa Romania Lohannis wamekuwa na mahusiano kwa miaka 60 na lengo la ziara hiyo ni kujenga mahusiano na ushirikiano kutokana na mazungumzo ya kimkakati ya kuwasaidia miaka ijayo.
“Kutafuta uhusiano na nchi za Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo, Tanzania ni nchi ya kimkakati tutashirikiana kujadili changamoto mbalimbali ambazo zinaikumba dunia,” amesema Rais Lohannis.
Ameongoza kuwa mazungumzo hayo yatachochea mahusiano katika kilimo, teknolojia, usalama wa wananchi na kuongeza nguvu katika nchini hizo mbili.
Wakati huo huo Marais hao, wameshuhudia utiaji saini wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama na Waziri wa nchi wa Masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Traian- Laurentiu Hristea.