Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Jamii imehimizwa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia mpangilio bora wa chakula na kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Akizungumza Novemba 11,2023 Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu, amesema magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto katika Bara la Afrika hasa kisukari na shinikizo la damu.
Dk. Ubuguyu alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa madhimisho ya Wiki ya magonjwa yasiyoambukiza iliyoandaliwa na Wizara ya Afya (Tamisemi), Mkoa wa Dar es Salaam na wadau wa huduma za magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa mujibu wa Dk. Ubuguyu katika kila watu 100 watano wana ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.
“Magonjwa yasiyoambukiza bado ni changamoto katika bara letu la Afrika hasa kisukari na shinikizo la damu. Kulingana na tafiti hata umri wa kuishi pia umepungua, kwa wanawake ni miaka 69 na kwa wanaume ni miaka 62 kutokana na changamoto mbalimbali,” amesema Dk. Ubuguyu.
Amesema baadhi ya watu wamezaliwa na magonjwa yasiyoambukiza kama vile sikoseli (selimundu) na kisukari ambayo yanaweza kuzuilika kwa kujilinda na magonjwa mbalimbali.
Mkurugenzi huyo amesema pia magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto katika umri wa wazee na kuwataka kuzingatia kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya zao.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Rashid Mfaume, amesema Wiki ya Magonjwa yasiyoambukiza Kitaifa mwaka huu itaadhimishwa mkoani humo kuanzia Novemba 14 hadi 18 ambapo kupitia wiki hiyo wananchi watapata fursa ya kupima magonjwa mbalimbali bure na kupatiwa ushauri wa kitaalamu.
Katika uzinduzi huo pia wazee kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam walishiriki kwa lengo la kujengewa uelewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.