27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake wataka mazingira rafiki uchaguzi 2024/2025 

Na Nora Damian, Mtanzania Digital 

Wanawake katika maeneo mbalimbali nchini wamependekeza kuwepo kwa mazingira rafiki na wezeshi ili washiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025. 

Takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi ikiwemo bungeni ambapo umeongezeka kutoka asilimia 31 hadi kufikia asilimia 37. 

Wanawake hao wameyasema hayo Novemba 8,2023 wakati wa warsha kuhusu ujenzi wa harakati katika kuhamasisha uongozi kwa wanawake, kukuza sauti zao na ushiriki katika siasa na nafasi za uongozi. 

Warsha hiyo ni sehemu ya Tamasha la Jinsia la 15 linalokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP). 

Eunice Limbu kutoka mkoani Shinyanga amependekeza Serikali iweke sheria ya kuwalinda wanawake wakati wa uchaguzi ili kuhakikisha kunakuwa na ushiriki mzuri wa kundi hilo. 

“Kura za maoni zisipigwe na watu wachache, zipigwe nje watu sahihi watajulikana na usawa wa kijinsia uzingatiwe,” amesema Eunice. 

Nuru Awadhi kutoka Dar es Salaam amependekeza kuwe na ukomo wa uongozi ili kutoa fursa kwa wanawake wengine kushika nafasi mbalimbali katika ngazi za maamuzi. 

“Kuwe na ukomo wa uongozi, watu wanabebana sana, bungeni wasipazoee maana kuna wanawake wengine ni wanafiki wanapambana kushusha wanawake wenzao walioko juu,” amesema Nuru. 

Rehema Mfaume kutoka Dar es Salaam amesema aliwahi kuwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa mwaka 2014 lakini wanaotoka katika vyama vya upinzani wanakutana na vikwazo vingi. 

“Wanawake tunapewa mbinu nyingi za kushiriki katika uchaguzi, tunapambana vya kutosha lakini tunarudishwa nyuma, kuna vikwazo vingi. Tunaomba Serikali itende haki bila kujali mtu anatoka katika chama gani,” amesema Rehema. 

Mwezeshaji katika wasrsha hiyo Deogratius Temba, amesema TGNP imekuwa ikishiriki kuandaa ilani za uchaguzi ambapo ilianza katika uchaguzi wa 2000, 2005, 2010, 2015, 2020 na sasa itazindua ilani ya uchaguzi ya 2025. 

“Ilani itakayozinduliwa Ijumaa (Novemba 10,2023) itagusa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, inawalenga wanawake ambao ni wapigakura na wenye nia ya kushiriki katika uchaguzi ili wawe sehemu ya mchakato huo,” amesema Temba. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles