Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imetumia zaidi ya sh. 2.5 bilioni (2,744,106,712.35) kununulia mtambo wa kisasa wa kufundishia katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI)
Mkuu wa chuo hicho, Dk.Tumaini Gurumo amesema mtambo huo (Crane Simulator) utasaidia kufundishia wanafunzi kwa vitendo na kuongeza thamani ya elimu inayotolewa katika chuo hicho pekee hapa nchini.
“Mtambo huu unasiadia kufundishia katika kozi ambazo utendaji kazi wake ni maeneo ya bandari, viwandani na migodini. Zaidi ya shilingi bilioni mbili nukta tano zimetumika kununulia mtambo huu mpaka kufungwa hapa chuoni,” amesema Dk.Tumaini.
Kwa upande wake mtaalamu wa mtambo huo, Elinathan Blasius, ambaye ni mkufunzi wa chuo hicho, mtambo ni muhimu kwa wanafunzi kwani utasaidia kupata elimu ya kuendesha mitambo mabalimbali.
“Mtambo huu una mada zaidi ya kumi hivyo kila mwanafunzi atapata elimu ambayo itamsaidia kuendesha mitambo mikubwa na midogo,” amesema Elinathan.
Naye mwalimu Leonard Mwesiga amesema kuwa mtambo huo ni muhimu sana kwa chuo hicho kwani unaweza kufundishia zaidi ya masomo sita na mwanafunzi akihitimu katika masomo hayo ataweza kuendesha mitambo ya aina yoyote katika sekta ya bandari,viwandani na migodini.