Na Gustafu Haule,Pwani
SERIKALI mkoani Pwani imeanza kuchukua hatua ya kufanya maandalizi juu ya kuwasaidia wananchi kuepukana na maafa yanayotokana na mvua za el nino kama ambavyo imetangazwa na mamlaka za Hali ya Hewa nchini (TMA).
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, ameanza kuchukua hatua hiyo leo Oktoba 19, katika Wilaya ya Rufiji kijiji cha Mohoro kata ya Mohoro akiwa na na timu yake ya kamati ya ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Michael Gwimile.
Amesema hatua ambayo tayari imechukuliwa ni pamoja na kuwahamisha wananchi wa Mohoro waliopo kandokando ya Bahari ya Hindi na kuwapelekea eneo mpya lenye mazingira mazuri ya kuishi hata katika nyakati za mvua.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho Kunenge amesema kuwa serikali imeona ianze kujipanga na kudhibiti maafa yanayotokana na mafuriko pindi mvua zinaponyesha kwa kuhakikisha wananchi wanawekwa katika mazingira salama.
Kunenge amesema wananchi hao wamepewa viwanja bure bila kulipia gharama yoyote na kwamba kila mmoja anapaswa kufanya maandalizi mapema ya kuanzisha makazi katika eneo hilo ambalo litakuwa limeondoa kero ya mafuriko yaliyokuwa yakitokea muda mrefu.
“Leo tumefika hapa kwa ajili ya kufanya maandalizi ya tahadhali juu ya mvua za el nino ambazo zimekuwa zikileta maafa kwa wananchi wetu na ukizingatia Mkoa wa Pwani umezungukwa na Bahari ya Hindi ambayo imekuwa ikijaa maji wakati wa mvua na hivyo kuleta athari kwa wananch,” amesema Kunenge.
Kunenge amesema kuwa kata ya Mohoro imegawanyika sehemu mbli ambayo ni Mohoro Mashirika na Mohoro Kaskazini na kuna kituo cha afya ambacho mwaka 2021/2022 kilikabiliwa na changamoto ya mafuriko lakini tayari serikali imelifanyia kazi jambo hilo.
Amesema eneo walilopata limetolewa na Wakala wa Usimamizi wa Misitu na Mazingira (TFS) ambapo ndani yake kunajengwa huduma zote za jamii ikiwemo kituo cha afya, shule, soko, makazi na mahitahi mengine .
Amesema kupatikana k wa viwanja hivyo imetokana na juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyeridhia kugawa eneo hilo kwa wananchi wake na kwamba hakuna budi ya kumshukuru kwa hatua hiyo kubwa.