25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

DCEA yateketeza hekari 807 za bangi

*Yakamata gunia 507 za bangi kavu, 11 wadakwa

Na Lulu Fau, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa, mgambo pamoja na vyombo vingine vya dola, imeketeza hekari 807 za mashamba ya bangi, imekamata gunia 507 za bangi kavu na watuhumiwa 11.

Akizungumzia tukio hilo leo asubuhi Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema operesheni hiyo maalum imefanyika mkoani Mara hususani katika kanda maalum ya Tarime Rorya kwenye bonde la mto Mara.

Amesema operesheni hiyo ilianzia Oktoba 2 hadi 8, mwaka huu na wamefanikiwa kukamata pia gunia 50 za mbegu za bangi pamoja na kuteketeza viwanda viwili vidogo vilivyokuwa vikitumika kuchakata na kufunga bangi kabla ya kusafirishwa.

“Wakazi wa eneo hilo wamelifanya bonde la mto Mara kama eneo maalum kwa ajili ya kilimo cha bangi na kujimilikisha kwa kutoruhusu mtu yeyote asiye mkazi kuingia kwenye bonde kama sehemu ya kuficha uhalifu wao na wanawatishia kumdhuru yoyote atakayeingia ndani ya bonde hilo bila ridhaa yao.

“Wamediriki kufunga ofisi ya kijiji wakimtuhumu mtendaji wa kijiji cha Nkerege kutounga mkono kilimo cha bangi.

‘‘Kitendo kinachofanywa na wananchi waliopo katika eneo la mto Mara ni kinyume na sheria, viongozi wa Serikali na wananchi ambao sio wakazi wa hapa hawaruhusiwi kuingia eneo la bonde,” alisema Lyimo.

Amesema uwepo wa daraja lililopo katika moja wapo ya vijito vinavyopeleka maji mto Mara, linatumika kama kizuizi cha watu kwenda kwenye hifadhi ya bonde la mto maeneo yanayolimwa bangi.

Ili mtu avuke anatakiwa kujieleza nia na madhumuni ya kuvuka kuelekea upande wa pili, na wahusika wasiporidhika na maelezo hawaruhusu kuendelea na safari.

Kamishna Jenerali Lyimo anaomba Wizara zinazohusika kushirikiana na Mamlaka kutokomeza kilimo cha bangi katika eneo hilo kwani mbali na operesheni iliyofanyika bado mashamba ya bangi ni mengi pembezoni mwa mto na wananchi wamekuwa wakitumia maji ya mto kumwagilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles