32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yakutana na wadau kujadili changamoto Sekta ya Utalii

Na Esther Mnyika Mtanzania Digital

Serikali imekutana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii kujadili changamoto zinazowakabili ikiwemo miundombinu huku ikiahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika nyanja hiyo.

Hayo yamebainishwa Oktoba 7, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki wakati akifungua kongamano la kujadili changamoto, mikakati na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta ya utalii Tanzania Bara na Visiwani kwenye maonyesho ya Saba ya S!te Swahili Internation Tourism Expo yanayoendelea katika viwanja vya Mlimani City.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya uwekezaji katika sekta ya utalii ili kuendelea kuvutia watalii wengi nchini na wataendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kukuza utalii wa ndani na nje.

“Pamoja ya changamoto ambazo tumezisikia hapa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano tutazishughulikia ili kuendelea kuboresha sekta hii muhimu yenye mchango mkubwa kwa taifa,” amesema Kairuki.

Amesema Serikali itakaa na Wizara za Uchukuzi Bara na Zanzibar ili kuangalia na kutafutia ufumbuzi changamoto ya usafiri inayowakuta watalii wanapotoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar na Zanzibar kwenda Dar es Salaam ikiwemo tozo wanazokutana nazo.

Aidha, amesema pamoja na changamoto zilizopo lakini idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 70,088 kwa mwaka 2021 hadi milioni 2.3 Juni, Mwaka jana.

Amesema ikiwa ndio mwaka wa kwanza tangu kuondoka kwa janga la uviko 19 idadi ya watalii wa nje imeongezeka mara dufu na kufikia watalii zaidi ya 1,454,000.

Amesema kutokana na kukua kwa sekta ya utalii Tanzania imekuwa nchi ya pili Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watalii na kwamba hiyo ni kwa mujibu wa Shirikia la Biashara la Utalii Duniani (WTTB).

“Haya mafanikio tuliyoyapata ni juhudi za Serikali zote mbili kwa kuwashirikiana kwa dhati na sekta binafsi na wananchi wote,”ameongeza.

Amesema uwepo wa kongamano hilo pia ni kuonyesha fursa zilizopo katika sekta ya utalii nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Damus Mfugale amesema wameweka mkazo katika maeneo matano ya kimkati ambayo yatasaidia kutangaza utalii nchini.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni utalii wa wanyama, utalii wa mikutano, utalii wa misitu, utalii wa tiba na utalii wa fukwe.

“Tumeweka nguvu kubwa kwenye kutangaza utalii kupitia maeneo hayo hivyo tunawaomba wawekezaji na watalii kujitokeza kwani kuna ardhi kubwa kuwekeza,” amesema Mfugale.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles