27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

St. Mary’s waweka mikakati kuboresha elimu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Uongozi wa Shule za St. Mary’s umejipanga kuendelea kuinua kiwango cha elimu nchini kwa kuhakikisha wanakuwa na mtandao wa shule hizo Tanzania nzima.

Kwa sasa St Mary’s wanamiliki shule 14 za msingi na tatu za sekondari zilizopo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mkurugenzi wa Shule za St Mary’s, Dk. Rose Rwakatare, akimpongeza Mwalimu Mkuu wa Shule ya St Mary’s Rwakatare Memorial iliyopo Mzumbe Morogoro, Elphas Kavusia, wakati wa mahafali ya awali na darasa la saba ya shule hiyo.

Akizungumza Agosti 19, 2023 Mkurugenzi wa shule za St. Mary’s, Dk. Rose Rwakatare, amesema wanaendeleza maono ya mama yao Dk. Getrude Rwakatare ya kukuza sekta ya elimu nchini.

Dk. Rose ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Morogoro alikuwa akizungumza wakati wa mahafali ya Darasa la Saba na Awali ya Shule ya St Mary’s iliyopo Mzumbe Morogoro.

“Tunawashukuru Watanzania kwa kuendelea kutuamini na kutuletea watoto, tunaiunga mkono Serikali katika kukuza sekta ya elimu nchini. Mwaka jana tulianzisha shule mpya mbili na malengo yetu ni kuweka mtandao wa shule zetu Tanzania nzima,” amesema Dk. Rose.

Pia amewaasa wazazi kuwa karibu watoto wao na kuwafunza maadili mema kuepuka mmonyoko wa maadili.

“Nawaomba wazazi tuangalie watoto wetu kwa karibu, mambo mengi yanaendelea kwa sababu hatuko karibu nao, mtenge muda wa kuongea na watoto, ukimfanya rafiki atakuambia mengi.

“Dunia imeharibika, kuna wimbi la mambo mengi machafu, kuna ushoga, usagaji, sisi kama wazazi kuanzia nyumbani tuwakemee, tuangalie utumiaji wa simu kwa watoto wetu, mambo mengine wanaiga, sisi sio Wazungu, sisi ni Waafrika tuna mila na desturi zetu.

Awali, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Elphas Kavusia, amesema mafanikio waliyoyapata tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2022 ni kuongezeka kwa wanafunzi.

Amesema shule hiyo ilianza ikiwa na wanafunzi 47 lakini kwa sasa ina wanafunzi zaidi ya 370.

Mkurugenzi wa Shule za St Mary’s, Dk. Rose Rwakatare, akizungumza wakati wa mahafali ya Darasa la Saba na Awali ya Shule ya St Mary’s Rwakatare Memorial iliyopo Mzumbe Morogoro.

Amesema pia wanafanya vizuri kwenye michezo na kwamba wana mpango wa kuongeza michezo zaidi kwa kuwa na uwanja wa kikapu na wavu ili kubaini uwezo wa watoto katika nyanja mbalimbali.

“Watoto wanashirikishwa katika utunzaji mazingira, tumeanzisha shamba darasa la mbogamboga ambapo wanajifunza kilimo kwa vitendo.

“Mwakani tunatarajia kuanzisha somo la Kichina na Kifaransa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya ulimwengu,” amesema Mwalimu Kavusia.

Mwalimu huyo amesema wanatarajia wanafunzi wote watafaulu mtihani wa taifa na kwamba wameweka malengo ya ufaulu mwaka huu kwa kupata wastani wa 273.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Katibu Tawala Wilaya ya Mvomero, Said Nguya, amewaasa wahitimu kujichunga na kujiepusha na tabia hatarishi ambazo zinaweza kusababisha wakatishe ndoto zao.

Mmoja wa wahitimu wa darasa la saba, Selina Kadilo, ameushukuru uongozi wa shule kwa malezi mazuri na kuahidi kuwa watafanya vema katika mtihani wa taifa.

“Haikuwa rahisi kufika hapa, lakini tumefika kwa msaada wa walimu wetu na Mungu. Kumcha Mungu na kujituma ndio msingi wa mafanikio…naamini tutafanya vema kwenye mtihani wa taifa,” amesema Selina ambaye pia alitunukiwa cheti cha uongozi bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles