*Yasema itasaidia kuzima mikopo ya kausha damu
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Kampuni ya Silverlands inayojihusisha na uzalishaji wa vifaranga na chakula cha kuku imesema inaanzisha mpango mahususi utakaoshirikiana na Programu ya BBT Mifugo kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha vijana na akinamama katika sekta ya ufugaji ili kukuza uchumi jumuishi na kupunguza mikopo kausha damu kwenye jamii.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 2, 2023 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akizindua mtambo wa kuangua vifaranga vya kuku katika hafla iliyofanyika mkoani Arusha.
“Mipango yetu katika tasnia ya kuku kwa sasa ni kuibadilisha kutoka kwenye ufugaji wa mazoea kwenda kwenye ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa wafugaji. Nawataarifu Watanzania wote kwamba sasa Silverlands wako na BBT kwa upande wa ufugaji kuku.
“Kwa msingi huo nawakaribisha na wawekezaji wengine wanofanya kazi hii ya kuku na wao kuungana na Serikali,” amesema Waziri Ulega.
Waziri Ulega ameeleza kwamba BBT inafanya vizuri kwenye upande wa mazao, ufugaji wa ng’ombe na samaki na hivyo anawakaribisha wawekezaji waingie pia kwenye ufugaji wa kuku ambao unapendwa zaidi na vijana na akinamama wengi.