Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko amekutana na wadau na taasisi mbalimbali wa madini kutoa na kupokea maoni ya marekebisho ya sheria na baadhi ya kanuni zake ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kikao kazi hicho kimefanyika Agosti mosi, 2023 jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Dk. Biteko amesema mchakato huo ulianza muda mrefu na kwamba wako hatua ya mwisho ya upokeaji maoni hayo.
“Ni vema tukutane na wadau wetu kabla maoni hayajasainiwa na waziri mwenye dhamana kuwapa mrejesho wadau wetu kabla hazijaenda kusainiwa na kufanyiwa kazi lazima tukubaliane,” amesema Dk. Biteko.
Amesema kwanza lazima wadau wajue hayo mambo wanayozungumza na iwapo maoni yao yamezingatiwa na kama hayakuzingatia tuwape sababu kwanini.
Amesema wametenga siku moja kwa ajili ya kupitia hizo kanuni imani yao watatoka na kanuni ambazo ni bora zaidi ili ziweze kuwasaidia wafanyabiashara.
Dk. Biteko akizungumzia kuhusu marekebisho ya kanuni amesema kanuni zipo nyingi kuna kanuni inahusianana na masoko ya madini na changamoto wanaziona ni katika eneo la adhabu.
“Mfano kuna kanuni ya uongezaji thamani ya madini ambayo imeamua kuanzisha leseni ndogo za uchenjuaji madini, hiyo mialo ambayo wanachenjua zamani ilikuwa watu wanafanya bila leseni,” amesema Dk. Biteko.
Ameongeza kuwa wameanzisha leseni ndogo pia ilikuwa watu wanajenga minala mahali popote kwenye makazi ya watu na kwamba kwa sasa wameamua kuweka mazingira mazuri zaidi na kusimamia.
Ameeleza kuwa wana kanuni nyingine ushiriki wa nchi kwenye uchumi wa madini na yapo maeneo wachimbaji wakubwa wana yalalamikia wanapokwenda kwenye masoko ya kimataifa wanakosa mtaji kwa sababu ya vipengele vilivyopo.
Aidha, amesema wanaangalia kwa pamoja waone ni kipengele gani ambacho watarekebisha ili kiweze kukidhi mahitaji ya wadau wao.
Naye Mwenyekiti wa Chemba, Mhandisi Philbert Rweyemamu amesema kongamano la maoni ni jambo muhimu kwa wadau wa madini na kwamba ni fursa.
“Changamoto zipo nyingi, tuliisisitiza Serikali kufanya marekebisho ya kanuni ili kutoa fursa kwa wachimbaji, leo tumefanya awamu ya kwanza bado siku mbili tutaendelea kutoa mapendekezo,” amesema Mhandisi Rweyemamu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi ya Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), Tariq James amesema wanashukuru Rais Dk. Samia Suluhu kwa kuona wadau wanapaswa kushiriki kutoa maoni ya mabadiliko mbalimbali ya sheria.