Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ametoa rai kwa watendaji wakuu wa wakala za Serikali kujitathimini utendaji kazi wao kama umekidhi malengo ya uwanzishwaji wake na kila wakala ina wajibu katika maeneo yake.
ASimbachawene ametoa rai hiyo leo Alhamisi Julai 27, wakati akifungua mkutano wa watendaji wakuu wa wakala za Serikali wenye lengo la kujadili mambo mbalimbali kuhusu wakala hizo ambapo amesema lengo la uanzishwaji wake ni kuisaidia Serikali katika utendaji kazi wake na kuhakikisha inachangia katika Pato la Taifa.
“Kuna baadhi ya wakala zinafanya vizuri na kuna baadhi zinafanya vibaya hivyo niwaombe wakala mjitathimini kama mmefikia malengo ya uwazishwaji wenu kabla hamjatathiminiwa na mtu,”amesema Simbachawene.
Amesema wakala zinapaswa kutumia mifumo ya Tehama katika utendaji wake ili kujenga utumishi mmoja na kwamba zinapaswa kushirikiana na wizara mama ili kujenga mifumo ili kuboresha utendaji.
“Hii mifumo inapaswa iwe shirikishi ili kurahisisha utendaji lakini pia wakala zote zinapaswa kuwa kidigital ambao bado amjaingia mnapswa kuingia na ambao mmeingia mnapaswa kuboresha hiyo miundombinu ili iwe shirikishi,”amesema Simbachawene.
Aidha, amewataka watendaji wakuu kuhakikisha wanawapeleka vijana kwenye mafunzo ili kuwaandaa kuwa watendaji bora wa baadaye na siyo kwenda wao kwenye mafunzo pindi yanapohitajika.
“Mimi niwaombe watendaji muwapeleke vijana kwenye mafunzo mara kwa mara kwani wao ndio wanaopaswa hasa kujifunza lakini sio nyinyi kule watapata exposure hao ndio watu mtakao waachia ofisi,” amesema Simbachawene.
Amesema katika utawala bora swala la maadili linapaswa kupewa kipaumbele hasa ukizingatia teknolojia imekua hivyo kujitahidi kutojihusisha na maswala ya rushwa kwani wao wanawakilisha serikali.
Naye, Katibu Mkuu Utumishi, Juma Nkome amesema wakala wameborasha huduma na kutanua wigo wa mapato hivyo ujitegemea wenyewe na kupata pesa za mfuko.
Amesema watendaji wakuu wanapaswa kutumia miongozo na mifumo mbalimbali iliyotolewa na wizara.
“Watendaji wakuu mnapaswa kutumia Tehama pia kutoa mchango stahiki kwenye pato la Taifa,”amesema Nkome.
Aidha, wameiomba serikali iwekeze katika wakala hizo ili ziweze kufanya kazi iweke miundombinu bora ili watimize majukumu yake.