22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

‘Faida Tanesco Sh Bilioni 109’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shirika la Umeme (Tanesco) limepata faida ya Sh bilioni 109.4 kutoka Sh bilioni 77 za mwaka 2021 ambalo ni ongezeko la aslimia 42.

Aidha mauzo ya umeme katika shirika hilo yameongezeka kutoka Sh trilioni 1.6 mwaka 2020/2021 na kufikia Sh trilioni 1.8 mwaka 2021/2022 ambayo yalikua kwa asilimia 11.

Sehemu ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na uongozi wa Tanesco na Msajili wa Hazina, Dar es Salaam.

Akizungumza leo Alhamis Julai 27,2023 wakati wa kikao kazi cha uongozi wa shirika hilo, Msajili wa Hazina na Wahariri wa vyombo vya Habari, Mkurugenzi wa Fedha Tanesco, Renata Ndege, amesema hali ya fedha katika shirika hilo inaendelea kuimarika na halitengenezi tena hasara.

“Mambo mengi yamevunja rekodi ambayo haijapata kutokea, sasa hivi tunapimana na ndio maana huduma imeboreka…hatujafika tunakotaka lakini huduma imeboreka sana,” amesema Ndege.

Naye Mkurugenzi wa shirika hilo, Maharage Chande, amesema bado lina malengo ya kusambaza umeme hivyo fedha zinazopatikana zinaelekezwa katika miradi ikiwemo kupeleka umeme mikoa mbalimbali.

“Mara nyingi unakuta kwamba tunapata faida lakini zile fedha tunatumia kuziwekeza katika miundombinu,” amesema Chande.

Aidha amesema kukamilika kwa miradi mbalimbali inayoendelea kutaongeza uzalishaji na kupunguza gharama ukiwemo wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao umefikia asilimia 90 huku wakitarajia kuwasha umeme Juni 2024.

Kwa mujibu wa Chande, kila mwaka huchagua wafanyakazi 20 wenye weledi kisha kuwapeleka nje ya nchi na kuwaunganisha kwenye kampuni kubwa ambapo 20 wanaendelea na mafunzo Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amelipongeza shirika hilo kwa maboresho makubwa na kushauri itafutwe tiba ya kudumu kwa matatizo mengine yanayolikabili.

“Kasi ya mabadiliko ndani ya Tanesco inaonesha taasisi hii imejipanga na inaweza kuwa ya mfano…Tanesco kutoka shirika la kupata hasara linastahili pongezi,” amesema Balile.

Shirika hilo lenye wateja milioni 4 kwa mwaka 2021/22 limefanikiwa kuwaunganishia umeme wateja wapya 504,366 huku upotevu wa umeme ukipungua kutoka asilimia 9 mpaka 8.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles