24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Kinyerezi waibua madudu ujenzi Daraja la Majoka

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Baadhi ya wananchi wa Mitaa ya Kifuru na Kibaga iliyopo Kata ya Kinyerezi ‘wamewaka’ kuhusu vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa daraja la Mto Majoka na kushauri usimamizi madhubuti kuepuka hasara inayoweza kujitokeza.

Vifaa walivyovibainisha ni mawe na mchanga waliodai unachimbwa kutoka katika mto huo.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Daraja la Mto Majoka linalounganisha Mitaa ya Kifuru na Kibaga.

Wakizungumza leo Julai 11,2023 wakati wa ziara ya Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kukagua miundombinu mbalimbali ya jimbo hilo, wamesema wanahofia daraja hilo kutokuwa imara kutokana na vifaa vinavyotumika.

Mmoja wa wananchi hao, James Kihiyo, alitoa mfano wa mawe yaliyomwaga kwamba hayana ubora na hata mchanga unakusanywa kutoka katika mto huo.

Aidha wakati wa ziara hiyo baadhi ya mafundi walionekana pembeni ya mto huo wakikusanya mchanga.

“Hata kama sisi sio mainjinia lakini ukitazama unajua, mfano ni jiwe lililowekwa hapo chini (anaonesha), ni jiwe la ‘ubuyu’. Tulichukua jiwe moja bila mtu yeyote kujua, tukaliloweka kwenye maji asubuhi tulikuta ni maji, sasa sijui kama injinia (Tarura) ulikagua ukaridhika nalo, au katika tender (zabuni) mliwaambia waweke mawe haya.

“Hata mchanga unaotumika ni wa hapa mtoni, kama ni fedha za wananchi zinatumika lazima tusimamie, umepewa kazi ukimaliza shida inabaki kwetu wananchi,” amesema Kihiyo.

Mwananchi mwingine ambaye pia ni mjumbe wa shina, Rashid Kasusula, amesema vifaa vinavyotumiwa na mkandarasi huyo havina ubora na kushauri usimamizi zaidi kuepuka hasara inayoweza kujitokeza baadaye.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Ilala, wameahidi kumsimamia mkandarasi huyo kuhakikisha daraja hilo linajengwa kwa ubora unaotakiwa.

Mhandisi kutoka Tarura Ilala, Legnard Mashanda, amesema daraja hilo litakalojengwa kwa miezi sita linagharimu Sh milioni 650 fedha kutoka Serikali Kuu.

Amesema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 13.2 utahusisha pia kusafisha mto mita 200 pande zote mbili, kuchonga barabara, kujenga mitaro ya pembeni mita 500, kujenga barabara ya maingilio kwa kiwango cha zege.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli (Wapili kulia), akikagua Barabara ya Tembomgwaza iliyojengwa kwa zege. Watatu kulia ni Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Ojambi Masaburi na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde.

Naye Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, ameitaka Tarura kumsimamia mkandarasi kuhakikisha daraja hilo linajengwa kwa viwango vinavyotakiwa.

“Tunategemea daraja lijengwe kwa standard (viwango), haya mawe nilishayasikia kuanzia kwenye ‘group’ na kuna mtu alinitumia, kwahiyo tunaomba injinia anayejenga jamani milioni 650 sio ndogo, hizi ni fedha za wananchi ambao wanalipa kodi ndiyo zinakuja kufanya maendeleo…kwahiyo tunategemea wananchi wapate kitu kizuri, naomba vigezo na masharti vizingatiwe.

“Leo nimekuja bado nimeona tu wanachimba, lakini nitapita saa yoyote hata usiku niangalie na ninaweza nikapita na mtaalam akaangalia,”amesema Bonnah.

Mbunge huyo pia amekagua Barabara ya Zimbili, Segerea – Bonyokwa, Majichumvi – Migombani zinazojengwa kwa kiwango cha lami na kusema malengo yao ni kufungua barabara zote za jimbo hilo kwa lami.

Pia amekagua Barabara ya Tembomgwaza iliyojengwa kwa kiwango cha zege sambamba na mfereji.

“Namshukuru sana mheshimiwa Rais Samia ametuletea miradi mikubwa katika jimbo letu, tunatengeneza barabara za lami hata kama ni fupi lakini tunataka ifikapo 2025 zote ziwe zinapitika kirahisi,” amesema Bonnah.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amempongeza mbunge huyo na madiwani kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kusema watahakikisha thamani ya fedha inakuwepo kwenye miradi yote ya maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles