Na Esther Mnyika mtanzania digital
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa wito kwa wadau mbalimbali wanaopata shida katika mfumo wa uombaji leseni kufika kwenye Banda lao lilipo kwenye maonyesho ya 47 ya biashara Sabasaba ili kasaidiwa kutatua changamoto hizo.
Akizungumza Julai 4, kwenye maonyesho hayo Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano BRELA, Roida Andusamile amesema wamejipanga kuhudumia wananchi na kutoa elimu mbalimbali ikiwemo umiliki ubunifu.
“Nchi imekuwa na wabunifu wengi ambao awafaidiki na bunifu zao kwa sababu ya kutokusajili bunifu hizo kuna watu wanabuni vitu vingi lakini hawajui kama kuna BRELA wangeweza kuja kusajili vumbuzi zao na kuzilinda kisheria na kuweza kunufaika nazo,” amesema Andususamile.
Amesema Taifa limekuwa na vijana wengi wasomi ambao wangeweza kujiajiri na kuajiri wengine kwa kutumia vumbuzi zao.
Amefafanua zaidi kuwa BRELA kwenye maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kumiliki leseni za biashara ndogo, kubwa na za kati ikiwemo viwanda.
“Kwenye maonyesho haya tunatoa elimu kwa umma jinsi ya kumiliki leseni zao za biashara na kujisajili kupitia njia ya mtandao lakini pia kuwaelewesha wananchi kuhusu brela na shughuli tunazofanya hivyo wananchi watutembee wapate elimu,” amesema Andusamile.