26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu: Mjadala wa Bandari usiligawe Taifa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mjadala unaoendelea kuhusu uwekezaji kwenye bandari ya Dar es Salaam usiligawe Taifa kwa sababu Serikali ya awamu ya sita ni sikivu.

“Mjadala unaoendelea kuhusu bandari ya Dar es Salaam usitugawe Watanzania. Usipelekee tukasambaratika. Tusitumie nafasi hiyo kutugawa kiitikadi, kidini au kisiasa. Sisi ni wamoja na jambo letu ni moja. Serikali yenu sikivu itaratibu haya,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 29, 2023 wakati akizungumza na mamia ya waumini waliohudhuria swala ya kitaifa ya Eid el Adh’haa iliyofanyika kwenye msikiti wa Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco, Kinondoni, jijini Dar es Salaam ambako alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali inapokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau na kwamba ina nia njema kuhusu suala hilo na ndiyo maana ililiweka hadharani.

“Natambua kuna watu wana hofu na umiliki wa bandari, ajira, ardhi na usalama wa Taifa lakini tusisahau kuwa TICTS wamekuwepo pale kwa miaka zaidi ya 22. Niwatoe hofu Watanzania kuwa malengo yetu ni kuboresha uchumi wa Tanzania. Tunataka watumiaji waliohama warejee,” amesema Mjaliwa.

Amesema Tanzania imezungukwa na nchi nane ambazo hazina bandari na zinategemea bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yao.

“Kwa hiyo bandari ya Dar es Salaam  ni kitovu cha uchumi. Mwekezaji huyu ana uzoefu mkubwa na teknolojia ya hali ya juu katika uendeshaji shughuli za bandari kwenye nchi 68. Sisi pia tunatamani kufanya vizuri kama yeye alivyofanya katika nchi nyingine,” amesisitiza.

Amesema yeye binafsi kwa kushirikiana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wataongoza suala hilo la utoaji elimu na anaamini kwamba Watanzania wataelewa malengo hayo na hasa hatua ambazo Serikali inatamani kuzifikia.

Waziri Mkuu ametoa ufafanuzi huo kufuatia ombi la Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhaj Nuhu Jabir Mruma la kuitaka Serikali iendelee kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu suala la uwekezaji kwenye bandari hiyo.

Mbali na umuhimu wa sikukuu hiyo, Waziri Mkuu alizungumzia pia masuala ya kudumisha amani na utulivu, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, udhibiti wa mmomomyoko wa maadili na utunzaji wa mazingira.

Aliwataka Waislamu nchini wanaposherehekea sikukuu hiyo, kila mmoja atambue wajibu wake wa kuwakumbuka masikini na wale wote wenye uhitaji kwa kutoa sadaka kwa masikini ikiwa ni sehemu ya ibada za Eid el Adh’haa.

“Siku ya leo tuitumie kuwakumbuka wale ambao hawajajaaliwa ili nao waweze kufurahi pamoja nasi. Tunapopata fursa ya kuchinja tuwakumbuke waja wote wenye uhitaji, yaani yatima, wajane, wazee na makundi mengine ya watu wenye uhitaji,” alisisitiza.

Akisisitiza umuhimu wa sadaka hiyo, Waziri Mkuu alisema: “Tutumie fursa hii kujitafakari sisi wenyewe ni kwa namna gani tunampa Mola wetu nafasi ya kwanza katika maisha yetu. Tukiona tumepwaya katika kujitoa, basi tuanze sasa kumpa Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza siku zote,” amesema.

Mapema, akizungumza na waumini hao, Kaimu Mufti, Sheikh Ally Khamis Ngeruko aliwataka viongozi wa dini hiyo waweke mipango ya kuwainua kiuchumi Waislamu nchini ili wanapokwenda kuhiji watafute pia fursa za kiuchumi.

“Viongozi wa dini tuweke mipango ya kuwainua kiuchumi, tufunue akili zao katika kupambana na kujiingiza kwenye miundombinu ya kiuchumi ambayo Serikali imewaandalia. Hijja ni fursa, kule Makka kuna soko la kimataifa, tuwahimize  wamachinga wa kimataifa waende kule na kupeleka bidhaa zetu.”

Alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihangaika usiku na mchana kutafuta wawekezaji ili kunyanyua uchumi wa Tanzania.

Naye, Alhaj Mruma akitoa salamu za BAKWATA, alisema sikukuu hiyo ni muhimu kwani inakumbusha siku ambayo waumini wenzao walikamilisha nguzo ya tano ya Uislamu ambayo ni Hijja.

Alisema BAKWATA itaendelea kuwaunganisha Waislamu nchini na kwamba inakemea vikali tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo limeikumba Tanzania na akahimiza malezi mema kutoka kwa wazazi na walezi.

Alisema Tanzania imekumbwa na wimbi la mmomonyoko wa maadili unaopandikizwa na tamaduni za kigeni likiwemo suala la ushoga. “BAKWATA tunaendelea kulaani sana na kukemea vitendo hivyo na tunaendelea kasisitiza kuhusu malezi mema ya vijana wetu ili kuwakuza katika maadili mema,” alisisitiza.

“Niwaombe wazazi wasimamie misingi imara katika familia zao ambako ni chumbuko la tabia njema linalotokana na malezi ya familia. Uislamu umehimiza tabia njema na umezingatia imani ya mtu kutokana na mema yake. Tukiyatekeleza haya kwa vitendo, tunaamini tutakuwa na kizazi chema ili kujenga Taifa ilililo imara na la watu waadilifu, wasio wala rushwa, wasio mafisadi na wenye kujali haki za wenzao.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles