Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa, amesema maoni yote yaliyotolewa na wananchi kuhusu makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji wa bandari yatazingatiwa.
Juni 10, 2023 Bunge lilipitisha azimio kuhusu makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Dubai Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.
Akizungumza Juni 16, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Msikate Tamaa Kata ya Vingunguti, amesema walipokea maoni mengi ya wadau wakielezea tahadhari zao mbalimbali wakitaka bunge liwe makini.
“Kuna kazi kubwa ya kuwaambia wana CCM na wananchi kile kilichofanyika bungeni na kuwaeleza mustakabali wa Bandari yao ya Dar es Salaam…yale yote wananchi waliyokuwa wanayasema yatazingatiwa,” amesema Silaa ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga.
Aidha amesema wanaopinga makubaliano hayo wako ambao hawajayaelewa na wengine ni washindani wa bandari hiyo ambao hawako tayari kuona Tanzania inafanikiwa.
“Kilicholetwa bungeni si mkataba, ni makubaliano ya awali yanayoenda kutengeneza msingi kama itakavyokubaliwa kwenye miradi mbalimbali.
“Nimepitia mara 19 katika vipengele vyote 31 hakuna hata neno moja la ‘sell, bandari haijauzwa, wanaosema haya wana nia mbaya na nchi yetu,” amesema.
Naye Naibu Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, amesema baadhi ya watu wanatumika kupotosha makubaliano hayo.
“Hii ni vita ya kiuchumi, nchi nyingine hazitaki kwa sababu tutakamata mizigo yote, Serikali haina mpango na wala haifikirii kuuza mali yoyote ya Watanzania,” amesema Zungu.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli ambaye pia ni mjumbe wa PIC, amesema hawajashiriki kikao cha uuzwaji bandari na kuwataka wananchi kuisikiliza Serikali.
Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abas Mtemvu, amesema mkutano kama huo utafanyika katika wilaya zote za mkoa huo kuwapa fursa wabunge kueleza kilichojiri bungeni na kuondoa sintofahamu kwa wananchi.
“Msisikilize maneno ya pembeni tafuteni wabunge wenu watawapa majawabu, msiingie kwenye mabishano, lolote likitokea mnayo haki ya kuwaita wabunge wenu.
“Tutakwenda wilaya zote ili wabunge wawafahamishe mambo mazuri yanayokuja,” amesema Mtemvu.