30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

GGML Kili Challenge-2023 kukusanya bilioni 2 kudhibiti VVU/UKIMWI

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KAMPENI ya GGML Kili Challenge inayoratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) mwaka huu inatarajiwa kukusanya dola za Marekani milioni moja sawa na Sh bilioni 2.3.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS), Dk. Leonard Maboko akizungumza katika hafla hiyo.

Fedha hizo ambazo hukusanywa kila mwaka, hulenga kuchangia juhudi za serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu yaani kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Hayo yamebainishwa jana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo katika hafla ya uzinduzi wa harambee ya uchangiaji wa fedha hizo kupitia kampeni hiyo ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2023.

Mbali na kuishukuru Serikali kwa kuunga mkono kampeni hiyo iliyoasisiwa mwaka 2002, Shayo alisema  wakiwa wadau wa mapambano haya ya UKIMWI na VVU, GGML imepokea msaada ambao uliiwezesha Kili Challenge kupiga hatua kubwa hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.

“Mwaka huu tumekuja tena kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo GGM kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) tunawakaribisha sana wadau wetu na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki kampeni hii.

“Kipekee tunapenda kutambua ushirikiano wa baadhi ya makampuni na taasisi mbalimbali ambazo tayari zimeshajitokeza kuchangia mfuko katika mwaka huu wa 2023. Nina imani wadau waliojitokeza leo watatusaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya kukusanya bilioni 2.3,” alisema.

Alisema VVU/UKIMWI bado ni tatizo kubwa nchini kwani takwimu za maambukizi mapya ya VVU haziridhishi, hususani kwa makundi maalum wakiwemo vijana.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Hassan Babu aliipongeza GGML na TACAIDS kwa kuendelea kuutumia mlima Kilimanjaro kama kivutio kinachotumika kukusanya fedha kwa ajili ya mwitikio wa VVU na UKIMWI. 

Alisema jambo hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika kuutangaza mlima huo maarufu duniani, na hivyo kuongeza idadi ya watalii. 

“Nakaribisha mawazo, ushauri kutoka kwenu na wadau wengine wa jinsi ya kuboresha zaidi kampeni hii,” alisema. 

“Natoa wito kwa watu binafsi, mashirika, taasisi na makampuni mengine kuiga mfano wa GGML kwa kujitoa zaidi kuchangia rasilimali za mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini, hususan katika kipindi hiki ambapo michango ya wahisani kutoka nje ya nchi inaendelea kupungua kwa sababu mbalimbali,” alisema.

Zoezi hilo la kupanda mlima linatarajiwa kuanza tarehe 14 Julai na kushuka tarehe 20 Julai mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles