26 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali imetenga Bilioni 9.9 ujenzi wa vituo saba vya zimamoto na uokoaji-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga Sh bilioni 9.93 katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa vituo saba vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Amesema kuwa vituo hivyo vitajengwa katika Mikoa ya Songwe, Simiyu, Kagera, Njombe, Manyara, Katavi na Geita.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano (Aprili 26, 2023) wakati akifungua vituo vya kisasa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vya Nzuguni na Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya miradi inayozinduliwa katika juma la kilele cha maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Vituo hivyo vimegharimu zaidi ya Sh bilioni 2.3.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa vituo hivyo pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha vitasaidia kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unakuwepo.

“Kukamilika kwa miradi hii kutasaidia kusogeza huduma za zimamoto na uokoaji karibu zaidi na wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za zimamoto na uokoaji kwa kufika eneo la tukio kwa wakati,” amesema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa miradi mingine inayotekelezwa na Serikali ni ujenzi wa Ofisi ya Kisasa za Jeshi la Zimamoto Temeke, Dar es Salaam, vituo vya polisi vya daraja A vya Kigamboni Dar es Salaam na Wanging’ombe mkoani Njombe.

Mingine ni Ofisi za Uhamiaji za mikoa ya Lindi na Geita na Ofisi za Makamanda wa Polisi katika Mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Unguja. “Miradi hiyo yote imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 16”.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kufanya maboresho makubwa na ya kiutendaji pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu ya Jeshi la Zimamoto yenye lengo la kuimarisha ufanisi katika utendaji wa jeshi hilo.

Aidha, Waziri Mkuu amelitaka Jeshi hilo lisimamie vizuri matumizi ya fedha za miradi zinazotolewa na Serikali ili kuharakisha mchakato wa utekelezaji wa miradi hiyo muhimu.

“Wasimamizi wa miradi inayotekelezwa hakikisheni kuna uwiano kati ya ujenzi wa miradi na thamani halisi ya fedha inayotolewa na Serikali”.

Kwa Upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kisasa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini ambavyo vitasaidia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi

“Katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita tunakwenda kushuhudia mapinduzi makubwa ya ununuzi wa vifaa katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo mchakato upo katika hatua za mwisho, tutanunua hadi helikopta za kuzimia moto,” amesema Mhandisi Masauni.

Naye,Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John William Masunga amesema Serikali imeendelea kutatua changamoto za jeshi hilo ikiwemo kununua boti za uokoaji majini, kuwezesha kupatikana kwa mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 4.9 kutoka Serikali ya Austria kwa ajili ya ununuzi wa magari 12 ya kuzima moto yakiwamo magari mawili yenye ngazi kwa ajili ya majengo marefu.

Ameongeza kuwa Serikali imeliwezesha Jeshi hilo kukamilisha ujenzi wa kituo kikuu cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Dar es Salaam katika eneo la Temeke: “Serikali pia inatekeleza Mpango wa Serikali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupata Vitendea kazi vya Dola za Kimarekani milioni 100,” amesema Masunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles