Na Pendo Fundisha, Mbeya
WATU watatu ambao majina yao hayajajulikana, wamekutwa wameuawa kwa kunyongwa kwa nguo shingoni na miili yao kuteketezwa kwa moto ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni, ya Mexico wilayani Kyela.
Inaelezwa kwamba watu hao waliwasili katika nyumba hiyo ya kulala wageni wakiwa wanne na mwanamke mmoja.
Inadaiwa kuwa mwanamume mmoja aliyetoweka, ni miongoni mwa waliotekeleza mauaji hayo.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Dk. Hashimu Mvogogo, alikiri kupokewa miili ya watu watatu, mwanamke mmoja na wanaume wawili.
Dk. Mvogogo alisema uchunguzi wa awali uliofanyika umebaini kuwa marehemu hao walinyongwa kwa nguo shingoni kabla ya kuchomwa moto.
“Saa tatu asubuhi (jana), nikiwa katika shughuli zangu, nilipokea taarifa kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hii, Francis Mhagama kwamba imepokelewa miili ya marehemu watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja.
“Baada ya kuchunguza imebainika kwamba watu hao waliuawa kwa kunyongwa na nguo shingoni na kuchomwa moto,” alisema Dk. Mvogogo.
Akizungumzia tukio hilo, mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni, Cyprian Mtengela, alisema wageni hao walifika juzi saa 10 jioni wakiwa wanne na kuchukua vyumba vya kulala.
Mtengela alisema watu hao walikuwa wakilalamika kwamba wamechoka kutokana na safari ya kutoka mjini Songea mkoani Ruvuma.
Alisema watu hao walichukua vyumba vitatu vya kulala; wanaume wawili walichukua vyumba namba 14 na 105 huku wengine wawili ambao walionekana kwamba ni mke na mume walichukua chumba namba 15, ambako ndiko kulikofanyika mauaji hayo.
“Chumba hiki namba 15 ndiko alikokuwa amelala mwanamke na mwanamume.
“Lakini mwanamume aliyelala na mwanamke huyu ambaye ni marehemu, ametoweka alfajiri ya leo (jana) na kutokomea kusipojulikana na kuaacha miili ya watu hawa watatu,” alisema Mtengela.
Alisema mwanamume huyo ndiye wanayemuhisi kuhusika na unyama huo kwa vile tangu siku walipowasili katika nyumba hiyo ndiye alikuwa akiwanunulia chakula na vinywaji hasa maji wenzake ambao walikuwa wamekusanyika chumba namba 15.
Mtengela alisema mwanamume aliyetoroka alijihimu alfajiri akisema kwamba anasafari huku akiwa ameshika mkoba mdogo na ndoo ya plastiki ambayo haikufahamika ilikuwa na nini.
“Unajua asubuhi ya leo (jana), mimi nilimfungulia mlango mtu huyu… alinieleza kuwa anasafiri na wenzie amewaacha ndani lakini watatoka baadaye.
“Baada ya hapo mimi nilikwenda kwenye shughuli zangu za kuuza pembejeo za kilimo na ilipofika saa mbili asubuhi nilifuatwa na watu na kunieleza gesti inaungua kwa moto,” alisema.
MTANZANIA ilipotaka kuona orodha ya majina ya wageni waliorodheshwa katika kitabu cha wageni, ilikuta majina yaliyokuwa yameandikwa yakiwa ni ya Hassani Ally, mkazi wa Visiwani Zanzibar kabila la Mtumbutu, Mariam Hassan Mngoni, Tatizo Adamu na Abbas Yasin, ambaye anadaiwa kuhusika na mauji hayo ya kinyama.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Francis Mhagama, alisema watu hao walifikishwa hospitalini hapo wakiwa tayari wamekwisha kufariki dunia.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba kabla ya kuchomwa moto, watu hao walinyongwa kwa kamba za nguo.
“Awali tukiwa kwenye eneo la tukio, tulishuhudia miili ya marehemu hao ikiwa imelala chini huku pembeni yao kukiwa na kamba za nguo zinazosemekana ndizo zilitumika kuwanyongea shingoni.
“Pembeni ya miili hiyo ilikuwapo mishumaa ambayo haikuwa inawaka lakini miili miwili ya mwanamke na mwanamume mmoja, ilikuwa imefunikwa mfuko wa rambo mweusi vichwani,” alisema.
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, kupata ufafanuzi kuhusu mauaji hayo hakupatikana.
Hata alipotafutwa kwa simu zake za kiganjani hakupatikana huku simu ikionekana kutokuwa hewani.