27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

RC Kunenge awatoa hofu abiria wanaotumia barabara ya Chalinze- Segera

Na Gustafu Haule, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakar Kunenge, amewatoa wasiwasi abiria wanaosafiri kupitia barabara ya Chalinze – Segera kuwa barabara hiyo kwa sasa ipo salama kutokana na juhudi za haraka zilizochukuliwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani (TANROADS) kudhibiti eneo la Kimange darajani lililovunjika kutokana na mvua mkubwa zilizonyesha.

Eneo hilo lililopo katika Kata ya Kimange katika Halmashauri ya Chalinze linalounganisha Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Nchi jirani lilikatika Aprili 15, mwaka huu na kusababisha adha ya msongamano mkubwa wa magari.

Kunenge ametoa kauli hiyo Aprili 18, 2023 baada ya kutembelea eneo hilo na kukuta tayari Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani (TANROADS) wamechukua hatua za haraka za ujenzi wa eneo hilo jambo ambalo limeleta faraja kwa watanzania wanaotumia barabara hiyo.

Kunenge, amesema kuwa wananchi wanaopanga kusafiri kupitia barabara hiyo waondoe hofu kwakuwa Serikali ya awamu ya Sita ipo kazini kufuatilia maeneo yote korofi na kwamba eneo la Kimange lililovunjika na kutoa hofu kwa wasafiri kwasasa limekamilika na lipo vizuri.

“Binafsi nitumie fursa hii kuwapongeza wenzetu hawa wa TANROADS kwa kazi waliyoifanya maana baada ya kutokea kwa tatizo hili la kuvunjika barabara hapa Kimange walifika maramoja na kuchukua hatua ndio maana hali ipo shwari na barabara inapitika,”amesema Kunenge.

Kunenge,amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga eneo hilo pamoja na kutoa taarifa za haraka kwa mamlaka za Serikali hasa pale wanapoona kuna tatizo limetokea katika maeneo yao.

Kwa upande wake meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage,amesema kuwa barabara hiyo ilivunjika Aprili 15, kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na kupelekea maji kujaa na hivyo kupitia juu ya barabara.

Mwambage , amesema baada ya kufika eneo hilo walifanya tathmini maramoja na kisha kuanza ujenzi Aprili 15 usiku na hivyo kulazimika kufanyakazi hiyo mchana na usiku na hatimaye kukamilisha Apriil 17 usiku.

Amesema,eneo lililokatika ni sehemu ya kipande cha daraja ambacho kilivunjika upande mmoja na hivyo kusababisha magari yote kupitia upande mmoja kwa foleni ambapo askari wa usalama barabarani walikuwa wakikesha kuongeza magari katika eneo hilo.

“Kutokana na hali ilivyokuwa na umuhimu wa eneo hili tumelazimika kujenga kwa kiwango cha zege na sasa tumekamilisha lakini tunatoa siku Saba za matazamio ili kusudi zege liweze kushika vizuri,”amesema Mwambage.

Hatahivyo, mhandisi wa ujenzi wa eneo hilo Baltazar Malamsha ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyojipange katika utekelezaji wa majukumu yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles