25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

TUCTA: Uwekezaji katika usalama na afya unalipa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) limetoa wito kwa maeneo ya kazi nchini kuzingatia taratibu zote za usalama na afya mahali pa kazi ili kulinda nguvukazi na mitaji iliyowekezwa jambo ambalo litapelekea tija kupatikana katika uzalishaji.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda, wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la TUCTA unaofanyika mkoani Morogoro (Machi 9 na 10, 2023) kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ikiwemo usalama na afya mahali pa kazi.

Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti, Takwimu, na Uhamasishaji wa OSHA, Joshua Matiko akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wajumbe wa Kikao cha Baraza Kuu la TUCTA.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkunda amesema maeneo ya kazi yanapokuwa salama na wafanyakazi wake kuwa na afya njema ni dhahiri kwamba shughuli za uzalishaji zitafanyika kwa ufanisi mkubwa hivyo tija kuongezeka.

“Usalama na afya katika maeneo ya kazi ni jambo muhimu sana kwetu sisi wafanyakazi na waajiri pia. Hivyo basi, tunapokuwa na mazingira salama kazini morali ya kufanya kazi inakuwa juu na hivyo kupelekea kujituma zaidi katika uzalishaji jambo ambalo lina faida kwetu sisi kama wafanyakazi na kwa wawekezaji pia,” alisema Hery Mkunda na kuongeza:

“Kikao hiki ni cha Baraza Kuu la Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchi nzima kutoka Taasisi binafsi na za umma hivyo tumeona kuna umuhimu mkubwa sana kwa viongozi hawa kupata elimu ya usalama na afya mahali pa kazi kwasababu wao ni wawakilishi wa wafanyakazi wenzao katika mambo mbalimbali vikiwemo vikao vya maamuzi ya utekelezaji wa masuala mbali mbali likiwemo suala zima la usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Mkunda.

Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti, Takwimu, na Uhamasishaji wa OSHA, Joshua Matiko akiwasilisha mada juu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi katika kikao cha Baraza Kuu la TUCTA unaofanyika mkoani Morogoro.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo,Utafiti, Takwimu, na Uhamasishaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Joshua Matiko, ambaye aliwasilisha mada ya usalama na afya katika kikao hicho, amesema elimu hiyo kwa viongozi hao imetolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taasisi ya OSHA wa kuyafikia makundi mbalimbali ya watu.

Aidha, ameeleza kwamba uelewa waliojengewa viongozi hao katika mkutano huo utawawezesha viongozi hao kujenga hoja kwa waajiri nchini ili kuboresha mazingira ya ya kazi katika sekta mbali mbali za kiuchumi.

“Viongozi hawa wa vyama vya wafanyakazi wanajukumu kubwa na muhimu la kutetea wafanyakazi wenzao katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la kuboresha mazingira ya kazi. Hivyo, ili waweze kutoa hoja zenye mashiko kwa waajiri wao ni lazima wawe na uelewa wa kutosha juu ya suala zima la usalama na afya. Matarajio yetu baada ya mafunzo hay ani kwamba watakaporudi katika maeneo yao ya kazi watafikisha elimu hii kwa wafanyakazi wenzao kupitia kamati za usalama na afya walizoziunda,” amesema Matiko.

Mjumbe wa Baraza Kuu la TUCTA akimuuliza swali mwasilishaji mada kutoka OSHA ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo,Utafiti, Takwimu, na Uhamasishaji, Joshua Matiko wakati wa Kikao cha Baraza Kuu la Viongozi wa wafanyakazi wa TUCTA mkoani Morogoro.

Aidha, viongozi na wajumbe wa baraza hilo wameishukuru sana OSHA kwa kutoa elimu katika kikao hicho na kukikiri kuwa elimu hiyo imewaongezea hamasa ya kuzingatia masuala ya usalama na afya huku wakiahidi kufikisha elimu hiyo kwa wafanyakazi wenzao watakaporejea katika maeneo yao ya kazi.

“Kimsingi nimefurahishwa sana na hii mada ya OSHA kwasababu sisi kama wawakilishi wa wafanyakazi inatusaidia kusimamia misingi ya usalama na afya katika maeneo yetu ya kazi na pia itakuwa chachu katika kuwahamasisha wale tunao wasimamia na kuwaongoza kwenye vyama vyetu. Nawasihi viongozi wote waliohudhuria kikao hiki kupeleka elimu hii kwa wafanyakazi ili waweze kuwa na uelewa wa namna gani wataweza kujikinga dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi” alisema Mkamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Tanzania (TUGHE), Jane Madete.

Kwa upande wake, Chrispin Ng’weng’we ambaye ni mjumbe wa Baraza hilo kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), amesema kuwa elimu hiyo imewajengea weledi wa kutambua haki zao

“Elimu hii imetutoa ukungu na kutujengea weledi juu ya mambo tuliyokuwa hatuyafahamu mfano baadhi ya wafanyakazi wanapata madhara wakiwa kazini lakini hawatambui haki zao hivyo basi sisi kama wawakilishi wa wafanyakazi tunalo jukumu la kuhakikisha elimu hii inawafikia wafanyakazi wenzetu,” alisema Chrispin Ng’weng’we.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles