25.6 C
Dar es Salaam
Thursday, December 5, 2024

Contact us: [email protected]

Mtaalamu: Lishe bora ni muhimu kwa watoto

Na Samwel Mwanga, Maswa

IMEELEZWA kuwa Lishe Bora ni jambo la muhimu sana na la kuzingatia kwa mtoto kwani ndiyo inayomfanya akue katika afya nzuri ya kimwili na kiakili.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Divisheni ya Afya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Adrorat Mpolo wakati akizungumza na wakinamama wa Kata ya Ipililo wilayani humo wakati wa siku ya Afya na Lishe katika Kijiji cha Ipililo.

Afisa Lishe wa wilaya ya Maswa, Abel Gyunda akitoa elimu ya Lishe bora kwa Wananchi wa Kijiji Cha Ipililo wilayani humo.

Amesema kuwa mtoto mdogo huhitaji lishe iliyo bora ili aweze kukua vizuri na awe na Afya njema pamoja na akili.

“Lishe iliyo bora ndiyo afya ya binadamu na akili inatengenezwa wakati wa utoto hivyo ni muhimu kuhakikisha tunawapatia watoto wetu chakula bora na siyo bora chakula”

“Kwa wilaya ya Maswa suala la chakula si tatizo kwani tuna choroko, viazi, karanga, mayai, maziwa pamoja na vyakula vingine ila tatizo letu ni moja hatuvitumii vizuri kwa kufuata Yale makundi matano ya Chakula,” amesema.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ipililo wilaya ya Maswa wakiangalia jinsi ya kuandaa uji wenye virutubisho kwa ajili ya watoto wadogo.

Dk. Mpolo amesema kuwa tatizo la kutotumia vizuri chakula kwa kufuata Lishe bora ndicho chanzo cha watoto kuwa na Udumavu hivyo amewataka wakinamama hao ambao ndiyo wenye jukumu la lishe kwa mtoto kuzingatia chakula bora Kwa mtoto.

Alisema kuwa kwa sasa udumavu kwa watoto bado upo kwa watoto katika wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu hivyo ni lazima kuwapatia watoto lishe bora Ili kuuondoa.

Naye Afisa Lishe wilaya ya Maswa, Abel Gyunda alisema kuwa kuna faida kubwa sana kwa mama kuweza kumnyonyesha mtoto wake walao kwa kipindi cha miezi sita.

Alisema kuwa kwa bahati mbaya hivi sasa watoto wengi wamekuwa hawapati virutubisho bora vinavyotokana na maziwa ya wazazi wao kwasababu kina mama wengi wamekuwa hawanyonyeshi watoto wao kama inavyotakiwa.

Aliongeza kueleza kuwa ni vizuri watoto hao sasa wakapikiwa uji ambao utakuwa na virutubisho mbalimbali ili kumwezesha mtoto kuwa na afya bora.

“Wakina mama wengine hawapendi kuwanyonyesha watoto wao wanawaachisha hata kabla ya miezi sita sita na wanawanywesha uji sasa leo tutajifunza kwa vitendo jinsi ya kuandaa uji wenye virutubisho kwa ajili ya watoto na wataunywa hapa hapa ili tuone tofauti na ule uji tunaopika huko majumbani,” amesema.

Baadhi ya wakinamama katika Kijiji cha Ipililo wilaya ya Maswa wakipewa uji uliotengenezwa kwa kuwekewa virutubisho mbalimbali Kwa ajili ya Afya ya watoto wao.

Naye, Esther Mboje ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ipililo alisema kuwa elimu ya lishe iwe inatolewa mara kwa mara kwani alikuwa haelewi mambo mengi juu ya kuandaa chakula bora cha mtoto licha ya kuwepo kwa aina mbalimbali za vyakula katika eneo analoishi.

“Hii elimu ya Lishe kwa kweli ni nzuri tuwe tunaipata mara kwa mara hasa katika kuandaa chakula bora cha watoto na mimi leo nimejufunza jinsi ya kuandaa uji wenye virutubisho kwa ajili ya mtoto wangu,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles