CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Meru mkoani hapa kimekiri nguvu ya aliyekuwa mgombea wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa, ndiyo iliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Meru, Furahini Mungure, mbele ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer, aliyeanza ziara ya kichama wilayani hapa jana.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Baraza la UVCCM na Kamati ya Utekelezaji wilaya hiyo, Mungure alisema pamoja na upepo huo kupita, CCM Meru bado wana nguvu kubwa.
“Tunajua Jimbo letu limeanguka kutokana na upepo wa Edward Lowassa. Sababu zote zipo wazi, kwani vongozi wa mila na dini walipewa maelekezo kuwa kura za Lowassa zimetosha hivyo watafute kura za Nassari,” alisema Mungure na kuongeza:
“Mbinu zilizotumika kulichukua tena Jimbo letu ni sawa na mchoro wa Entebe nchini Uganda wakati wa vita pale askari wa Israel walipomwokoa Muisrael mwenzao kwa dakika 92 tu. Ndicho kilichofanywa kwenye jimbo letu, lakini bado hatujakata tamaa, tunaendelea kujipanga,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Laizer alisema nia ya CCM kwa sasa ni kuimarisha umoja baaada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Alisema jambo moja ambalo viongozi na wanachama wanapaswa kulifanya ni kusameheana na kuendelea kuvumiliana kwa kila mmoja wao.
Ikiwa ziara yake ya kwanza tangu achaguliwe katika nafasi hiyo, Mwenyekiti wa Mkoa, Laizer alisisitiza kwamba umefika wakati watumishi wa serikali kutambua kuwa wanafanya kazi chini ya Serikali ya CCM.
Laizer ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Longido kabla hajastaafu, aliwaambia wajumbe hao kwamba hafanyi kazi za chama kwa lengo la kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa 2017.