29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yawapa faru majina ya Waziri Mkuu na Balozi wa Ujerumani

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wizara ya Maliasili na Utalii imewatangaza Faru wawili na kuwapa majina ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Regine Heiss.

Hatua hiyo imefikiwa leo Desemba 20,2022 jijini Dar es Salaam katika hafla ya makabidhiano ya magari 51 aina ya Land Cruiser yenye thamani ya Sh bilioni 15 yaliyokabidhiwa kwa Waziri Mkuu Majaliwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya mradi wa Msaada wa Dharula kwa uhifadhi na utalii Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi, Pindi Chana amesema Faru Majaliwa alizaliwa Januari, mwaka huu huku Faru Heiss alizaliwa Februari, mwaka huu ambao ni zao la Faru Rajabu.

Balozi Chana baada ya kufanikisha hatua hiyo ya kuwapa majina ya Waziri Mkuu na Balozi wa Ujerumani, wadau wengi wameonesha kuhitaji na wao majina yao yatumike kwa wanyama wengine ambapo ametoa wito kwa kila mwenye kuhitaji kufika Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili aweze kuchangia hatua hiyo.

Magari hayo ambayo pia yalikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ni msaada wa dharula kwa uhifadhi na utalii katika mbuga za Serengeti, Nyerere na Selous ambapo yatatumika kwa ajili ya kufanyia doria, kuleta ujirani mwema na kuimarisha mawasiliano ndani ya mbuga hizo.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri Mkuu Majaliwa, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amefurahishwa na jitihada za Wizara ya Maliasili na Utalii na ameipokea kwa furaha taarifa hiyo ya msaada kutoka nchini Ujerumani.

“Rais Samia ana matumaini kwamba uhusiano wa Tanzania na Ujerumani utaendelea na anaamini Wizara ya Maliasili na Utalii na bodi zake zinafanya vizuri na jitihada zenu zitakuwa endelevu na kuifanya iwe ya ushindani zaidi.

“Nataka nimtoe wasiwasi Balozi Regine Heiss kuwa awe na amani magari hayo yatatumika kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii pekee wala hayatapelekwa kwenye wizara nyingine,” amesema Majaliwa.

Amesema pia Serikali ya Tanzania ipo kwenye mchakato wa kununua ndege moja na Helkopta kwa ajili ya kupambana na majanga mbalimbali lakini pia wataendelea kushirikiana na jumuiya za kimataifa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi.

“Ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria ambao uliasisiwa na baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere ambao umekuwa ukibadilika kulingana na nyakati,” amesema Majaliwa.

Nae Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Heiss amesema anafuraha kukabidhi magari hayo kwa serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya utalii hapa nchini.

“Novemba, mwaka jana Ujerumani ilikaa na kuangalia jinsi ya kuisaidia Tanzania katika sekta ya utalii kwa kukabiliana na ujangili, mabadiliko ya tabianchi na kuangalia matumizi bora ya ardhi kwa kuondoa mimea vamizi, hivyo msaada huu ni matokeo ya tathimini hiyo iliyofanyika,” amesema Balozi Heiss.

Ameongeza kuwa amefurahi kuona serikali ya Ujerumani na Tanzania zimeunganisha nguvu pamoja kupambana majanga mbalimbali yanayoikumba sekta ya utalii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles