Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Maji Jumaa Aweso leo Novemba 6, 2022 ametembelea hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha huduma za maji ndani ya hospitali hiyo zinaendelea kuwepo na kuweka mipango mizuri kwaajili ya baadae.
Katika ziara hiyo Waziri Aweso ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Antony Sanga.
Waziri Aweso ameagiza DAWASA ihakikishe inapeleka maji ya uhakika kwa sasa na kusaidia uwekaji wa maji ya akiba kama tahadhari kwa baadae.
Aidha Waziri Aweso ameelekeza Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kutafiti haraka na kuchimba kisima ili kuwa na uhakika wa upatikanaji Maji.
Katika hatua nyingine, Akitoa taarifa ya upatikanaji wa maji katika hospitalini hapo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi alieleza umuhimu wa kuwa na akiba ya maji ndani ya Hospitali zote nchini ili kuepusha usumbufu wowote kwa huduma za tiba kwa Wananchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbil,i Prof. Janab Mohammad amefafanua kuwa Hospitali inahitaji angalau akiba ya lita milloni sita (6).
Mwisho, Waziri Aweso ameagiza Wizara ya Maji kutenga na kuleta fedha kwaajili ya Tenki kubwa la kuhifadhi Maji Muhimbili katika kuhakikisha huduma ya Maji inakua ya uhakika wakati wote.