29.1 C
Dar es Salaam
Sunday, December 15, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Lugomela aridhishwa na ujenzi wa bwawa la maji Zebeya wilayani Maswa

Na Samwel Mwanga,Maswa

MKURUGENZI Wa Raslimali za Maji, Wizara ya Maji, Dk. George Lugomela amekagua ukarabati na ujenzi unaoambatana na  upanuzi wa bwawa la kuhifadhi maji ya mvua katika kijiji cha Zebeya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu na kuridhishwa  na maendeleo ya kazi hizo zinazofanyika.

Mkurugenzi wa Raslimali za Maji,Wizara ya Maji, Dk. George Lugomela(mwenye miwani)akitoa maelekezo ya kukamilishwa kwa ujenzi wa bwawa la Zebeya katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea ujenzi wa bwawa hilo.(Picha Na Samwel Mwanga)

Bwawa hilo linafanyiwa ukarabati na upanuzi kwa thamani ya Sh milioni 754 chini ya Wizara ya Maji kupitia Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria.

Akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Maswa,Dkt Lugomela ametembelea eneo la ujenzi wa bwawa hilo katika kijiji hicho na  amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo ambao ni moja ya miradi mingi mikubwa hapa nchini ambayo itakuja kuwa na matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi wanaolizunguka bwawa hilo.

Dk. Lugomela amesema bwawa hilo litakapokamilika  litafanikisha kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho na Kata ya Senani.

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeigiza Wizara ya Maji kupitia kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha inachimba mabwawa kwa kila wilaya hasa zenye ukame ikiwemo wilaya hiyo ili kutatua changamoto hiyo na kuongeza njia za kukuza uchumi wa maeneo husika.

“Huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo inatutaka hadi kufikia mwaka 2025 tuwe tumechimba walao mabwawa mawili kila mkoa ila kwa maeneo yenye ukame tunaweza kuongeza idadi ili kuwaondolea changamoto ya maji wananchi kwa mfano wilaya ya Maswa ni kame tunachimba mabwawa mawili hili la Zebeya na baadaye tutachimba la bwawa katika kijiji cha Ilambambasa,” amesema Dk.Lugomela.

Amesema kuwa walitegemea ujenzi wa bwawa hilo kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu Oktoba mwaka huu ila kutokana na changamoto ya mitambo ya ujenzi kuharibika mara kwa mara amemwagiza Mhandisi wa Ujenzi wa Bwawa hilo,Edward Malale anakamilisha kabla ya musimu ya mvua kuanza mwishoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu.

“Mhandisi ongeza kasi ili mvua zitakapoanza kunyesha zijaze bwawa hili maana tunahitaji lianze kuwahudumia wananchi mwaka huu pamoja na changamoto ya  mitambo kuharibika sasa nimeona kazi inakwenda vizuri hivyo mfanye kazi usiku na mchana kamilike,”amesema.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo,Mhandisi wa Ujenzi wa bwawa hilo, Edward Malale amesema kuwa  hadi sasa kazi zilizofanyika ni pamoja na kuchimba na kutoa tope, ujenzi wa tuta na kujenga miundo mbinu ya kutolea maji kwenye bwawa.

Amesema kuwa  matokeo ya ukarabati huo ambao umefikia aslimia 90 utaongeza ujazo wa bwawa zaidi ya asilimia 50 ya uwezo wake wa awali na sasa litakuwa na ukubwa wa mita za Ujazo 90,000 na ifikapo mwezi Novemba 15 mwaka huu ujenzi huo utakuwa umekamilika.

“Tumeondoa tope na lengo bwawa hili liweze kujaza maji mara mbili ya ilivyokuwa awali sasa mita za ujazo 90,000 zitaingia,tuta litakuwa na ukubwa wa mita tano pia tutajenga sehemu ya utoro wa maji ili bwawa likijaa liweze kupumua sambamba na kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo maji na vituo vya kuchotea maji nje ya bwawa hivyo hatutegemei kwa mtu au mifugo kuingia bwawani kutafuta maji,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria,Meigaru Mollel amesema kuwa ukarabati wa bwawa hilo ulioanza Septemba 17 mwaka huu ukikamilika utanufaisha watu 11,671 na Mifugo 3430 na kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji katika kijiji hicho.

Amesema pamoja na serikali kuona umuhimu wa ukarabati wa bwawa hilo lakini bado kuna changamoto kubwa ya baadhi ya shughuli za kibinadamu zikiwemo makazi ya watu,kilimo na ufugaji zinafanyika ndani ya hifadhi ya bwawa hasa kwenye dakio la maji yanayoingia kwenye bwawa hivyo kwa sasa wataweka mipaka ya kuhifadhi eneo la bwawa hilo ili liweze kuwa endelevu.

Bwawa la Zebeya lilijengwa mwaka 1950 lakini kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu lilijaa tope na kukauka wakati wa kiangazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles