26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi CCM Rukwa wazichapa kavukavu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukala, anadaiwa kumtwanga mangumi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) katika mkoa huo, Ramadhani Shabani.

Hali hiyo ilitokea juzi Septemba 20, 2022 saa nane mchana katika ukumbi wa RRC Sumbawanga, ambapo kikao cha kujadili majina ya wagombea nafasi ndani ya chama hicho kilifanyika.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, chanzo cha kutwangana ngumi kati ya viongozi hao wa chama hicho tawala ni kupishana kauli baada ya kukatwa jina la mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenezi Wilaya ya Sumbawanga vijijini.

“Chanzo kilikuwa ni kushutumiana kupokea rushwa na kurushiana maneno, ndiyo mwenyekiti wa mkoa akatoka jukwaa kuu na kumfuata huyo wa UVCCM wakaendelea kubishana na baadaye huyo wa mkoa akamtandaka miguuni huyo wa UVCC,” kilisema chanzo hicho.

Alisema kwa desturi ya chama hicho, nafasi za uongozi huombwa kuanzia chini na kujadiliwa na vikao mbalimbali kabla ya uchaguzi wenyewe.

Alisema katika tukio hilo, kikao kilikuwa kinajadili nafasi ya uenezi wa chama hicho Wilaya ya Sumbawanga vijijini, awali Sekretarieti ya chama hicho ndani ya wilaya hiyo ilipitisha majina matatu kugombea nafasi hiyo na yalivyofika kwenye Kamati ya Siasa wilaya, jina moja likakatwa.

Alisema Sekretarieti ya Mkoa ilivyokaa, ilirudisha jina lililokatwa na mchakato ukaendelea kwenye Kamati ya siasa ya Mkoa ambayo ilipitisha majina kama yalivyoletwa na sekretarieti ya Mkoa.

Alisema Halmashauri Kuu ya mkoa ilipokaa, jana chini ya, Lukala ambaye ndiye pia alikuwa kiongozi kwenye kamati ya siasa mkoa, alionekana kutaka kuyageuka maamuzi yake ya awali.

“Hapo sasa ndipo shida ilipoanzia, watu wakawa wanahoji kwanini mwenyekiti anataka kula matapishi yake, ni kitu gani kimetokea,” alisema.

Alisema baada ya hali hiyo, shutma za kupeana rushwa zilizidi, ambapo upande mmoja ulikuwa unadai wanaotaka jina lisikatwe wamekula rushwa na upande mwingine unasema wanaotaka kukata jina wamekula rushwa za Sh 50,000.

Alisema katika hali hiyo, mwenyekiti wa UVCCM alisimama na kuhoji kwanini wajumbe waliopitisha majina kwenye Halmashauri ya Mkoa sasa wanataka kupindua maamuzi yao wenyewe.

Katika hali isiyo ya kawaida, inadawa mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa alishuka jukwaani na kumfuata mwenzake wa UVCCM na kuendeleza mabishano ambapo mwishoni alimrushia Makonde.

Hali hiyo ilifanya kikao hicho kuvunjika kwa muda na kurejea baadaye baada ya usuluhishi kufanywa.

“Tulivyorudi ndani, mwenyekiti wa mkoa alitaka huyo wa UVCCM atoke nje, yule kijana aligoma akisema yeye ni mjumbe halali wa hicho kikao na hawezi kutoka labda apewe barua rasmi,” kiliendelea kupasha chanzo chetu.

Baada ya mzozo huo, Halmashauri Kuu ya chama hicho, iliamua Kamati ya Siasa Mkoa yote ipelekwe kwenye kamati ya maadili wachunguzwe juu ya tuhuma za rushwa walizotoleana.

Akizungumza na Mtanzania Digital Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Rukwa, Ramadhan Shaban amesema kuwa amekili kupigwa na Mwenyekiti huyo huku akisema kuwa Chama (CCM) ina utaratibu wake wa kushughulikia matatizo nakusisitiza kuwa jambo hilo ni siri.

“Siyo kwamba tulipigana bali mimi ndiye nilipigwa makonde na Mwenyekiti wangu sababu alitoka kwenye meza yake akanifuata, lakini pamoja na hayo, chama kina utaratibu wake wa kushughulikia mambo kama hana ndiyo sababu hata sisi viongozi tumeapa kulinda siri za chama kama ikijumhisha vikao.

“Hivyo, hata hili lililotokea linabaki kuwa siri kwa kuwa lilitokea ndani ya chama chetu na taratibu zake za kushughulikia masuala kama haya, mimi kama kiongozi ni wajibu wangu kulinda siri za vikao japo naweza kusema kwamba hilo jambo lilitokea lipo,” amesema Shaban.

Mtanzania Digital imemtafuta Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukala kuhusu taarifa hizo ambapo amesema kuwa hata yeye anaziona taarifa hizo katikamitandao ya kijamii na hajui zimeanzia wapi.

“Namimi naziona kwenye mitandao ya kijamii na sijui zimeanzia wapi na sijui hata aliyezisambaza analengo gani, ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho,” amesema Lukala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles