29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ukerewe yapata mwarobaini wa migogoro ya ardhi katika taasissi za umma na wananchi

Na Clara Matimo, Ukerewe

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Emmanuel Sherembi amesema halmashauri hiyo inaendesha zoezi la upimaji ardhi kwenye maeneo ya taasisi za umma ili yatambulike kisheria na kupatiwa hatimiliki.

Akizungumza na Mtanzania Digital Agost 14, 2022 Sherembi amesema lengo la kuendesha zoezi hilo la upimaji wa ardhi katika maeneo ya taasisi za umma ni kuepusha migogoro ya ardhi baina ya serikali na wananchi ambao huvamia maeneo hayo na kuanzisha shughuli za kibinadamu.

Wataalamu wa upimaji ardhi kutoka Arimo, ofisi ya kamishana wa Ardhi Mkoa wa Mwanza na halmashauri ya Ukerewe wakiendelea na zoezi la upimaji katika moja ya taasissi za serikali katika halmashauri hiyo.

Amesema zoezi hilo ambalo watalifanya kwa siku 49 wamelianza tangu Julai 22, mwaka huu wanalifanya kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo na Upimaji wa Ramani  Morogoro (Arimo), ofisi ya kamishna wa ardhi mkoa wa Mwanza na wataalamu wa ardhi wa halmashauri ya Ukerewe.

“Tunashirikiana na chuo cha Morogoro ambao tayari wametupatia wanafunzi ikiwa ni sehemu ya vitendo ya kujifunza lakini pia watafanya kazi hii ya upimaji, tutahakikisha maeneo yote ya taasisi za serikali kwa maana ya shule zote za msingi, sekondari, vituo vya afya, zahanati, maeneo yote ya vijiji na kata yote yanapimwa.

“Na lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaondoa migogoro ya ardhi na mwingiliano unaofanywa na wananchi katika kuingilia maeneo ya taasisi za serikali na hii moja kwa moja ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi lakini pia maagizo ya viongozi wetu wa nchi akiwemo mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,”amesema Sherembi.

Kiongozi wa msafara wa wataalamu kutoka Taasisi ya Mafunzo na Upimaji wa Ramani  Morogoro, Colman Charles, amesema”Nimekuja Ukerewe na timu ya vijana 17 tutakuwa tunasimika alama za mipaka kwa maana ya bicons, tutakuwa tunachukua taarifa za kijiografia, tutakuwa tunachora ramani na kuandaa mafaili kwa ajili ya kupewa hati lengo ni kuziepusha taasisi hizi na migogoro mbalimbali ya ardhi.

“Wazo la project hii au mradi huu lilitoka Muleba, Mkurugenzi wa Ukerewe Emmanuel Sherembi alikuwa huko na chuo kiliwahi kumpatia vijana kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili kwa hiyo alipohamia ukerewe akaona zoezi hili alifanye hapa,” ameeleza Charles.

Mpima Ardhi kutoka Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Mwanza, Paulo Ntunguru, amesema ofisi hiyo imetoa vifaa vya upimaji ardhi vya kisasa kwa ajili ya kurahisisha zoezi la upimaji wa taasisi za serikali katika halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili ziweze kumilikiwa kisheria na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo inaweza ikajitokeza kwa sababu maeneo mengi ya taasisi za umma yamekuwa yakivamiwa.

Kwa upande wao Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe, Joshua Manumbu pamoja na Diwani wa Kata ya Nakatunguru, Boniphace Mataba wamesema upimaji huo utasaidia sana kulinda ardhi za taasisi za serikali kwani baadhi ya wananchi ambao huvamia maeneo hayo watatambua mipaka ya taasisi hizo hivyo kutozivamia.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nebuye Kata ya Ngoma Wilaya ya UkereweBenedicto Malima,amemshukuru Mkurugenzi  Sherembi kwa kuwapalekea timu ya wataalamu wa kupima mipaka ya shule ya Msingi Nebuye kwani baadhi ya wananchi ambao wako jirani na shule hiyo wamekuwa wakivamia na kufanya shughuli za kibinadamu.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nebuye ambako ni miongoni mwa maeneo ambayo zoezi hilo limefanyika akiwemo Felister Sulusina John Sesejawameipongeza serikali kwa hatua hiyo ambayo inamanufaa ambapo wamesema itawaondolea migogoro ya ardhi  na serikali.

Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Ardhi Wilaya ya Ukerewe, Paschal Malecha, jumla ya Shule za msingi 158, sekondari 28, vituo vya afya 38, ofisi za kata 25, za vijiji 71 zitapimwa na kupatiwa hati miliki.

“Vilevile maeneo mengine yatakayopimwa ni viwanja vya michezo vya vijiji, maeneo ya misitu, maeneo ya vijiji ambayo yanamiradi ya serikali lakini mbali  ya upimaji wa maeneo ya taasisi za umma, halmashauri  ya Ukerewe tumejiwekea malengo ya kupima viwanja 500 kwa mwaka huu wa fedha  kwa ajili ya makazi ya wananchi ili kuepuka ujenzi holela,” amesema Malecha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles