Na Mwandishi Wetu, Lindi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa Sh bilioni 54 kwa ajili ya kugharamia mradi wa maji wa Chiuwe utakaohudumia wilaya za Ruangwa na Nachingwea.
Ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Julai 4, 2022) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Mchenganyumba, Mbecha na Chimbila ‘B’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya ya Ruangwa.
Majaliwa alisema maeneo mengi ya wilaya hiyo maji yake ni ya chumvi, hivyo Serikali ilifanya utafiti na kubaini kuwa chanzo cha maji cha Chiuwe maji yake hayana chumvi na ni ya kutosha kuweza kuhudumia vijiji vya wilaya hiyo na wilaya jirani ya Nachingwea.
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kitakachowezesha kutekelezwa kwa mradi huo ambao kukamilika kwake kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo.
Vilevile, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania wote kujiandaa kuhesabiwa ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa sensa na viongozi kwenye maeneo wanayoishi. Zoezi hilo limepangwa kufanyika nchini kote Agosti 23, 2022.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wa wilaya ya Ruangwa Mhandisi Lawrence Mapunda alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza itahusisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 21 vya wilaya ya Nachingwea.
Mhandisi Mapunda alisema ujenzi wa mradi huo ambao unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 utakamilika mwaka 2025/2026.
“Kwa sasa utekelezaji wa mradi huu upo katika hatua ya manunuzi na unatarajiwa kukamilika baada ya miaka mitatu kwa awamu zote.,” amesema.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza tatizo la upatikanaji maji wilayani Ruangwa kwa zaidi ya asilimia 80. Chanzo cha maji cha Chiuwe kilichopo Nyangao kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 15 kwa siku huku mahitaji ya wilaya ya Ruangwa kwa siku ni tani milioni tisa.