*Ni za matumizi ya zaidi ya Sh bilioni 1.5
Na Clara Matimi, Ukerewe
Imebainishwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza haijajibu hoja ya matumizi ya zaidi ya Sh bilioni 1.6 ambazo ilikopa kutoka Akaunti ya Amana bila kuwa na idhini kwenye hati za malipo.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na haijawahi kutekelezwa licha ya halmashauri hiyo kutakiwa kufanya hivyo kila mwaka ili ifungwe.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Juni 28, 2022 na Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje (CAG) Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani, kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani uliolenga kujadili hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na utekelezaji wake ambapo hoja kubwa iliyojitokeza ni matumizi ya fedha hizo ambazo hazina vielelezo.
Kwa mujibu wa Shabani, mwaka wa fedha 2020/2021 halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ilipata hati inayoridhisha huku akifafanua kwamba hoja 38 sawa na asilimia 39 hazijatekelezwa ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji huku 10 sawa na asilimia tisa zikiwa hazijatekelezwa kabisa.
Baada ya kuibuka hoja hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameiagiza timu maalumu ya kuchunguza ubadhilifu wa fedha za umma kwenye halmashauri ya Buchosa na Kwimba aliyoiunda alipoanza ziara ya kujadili hoja za CAG katika halmashauri zote Juni 20, kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika kukopa fedha hizo kwa Ukerewa na namna zilivyotumika.
“Nataka kupata majibu ya hizo fedha kiasi cha Sh bilioni 1.63 hata kama ziliibwa ni jibu, kama ni mtu wa kukamata ni jibu, nawahakikishia kama kuna mtu atakayepatikana wa kufungwa afungwe lakini afilisiwe kwanza fedha irudi kwa ajili ya hamashauri hii, mashaka yamekuwa ya nini kwa miaka yote hiyo kama fedha ilitumika vizuri na vielelezo vipo si vipelekwe kwa CAG.
“Ukiona hoja inakaa kwenye kablasha na maelezo ya hoja hiyo ni miongoni mwa hoja ambazo haziko kwenye utekelezaji hazina majibu kwa CAG tangu 2017/2018 hadi 2020/2021 hakuna majibu ujue kuna shida hapo kuna watu wamejinufaisha na hilo halikubariki,”amesema na kuongeza:
“Sasa menejimenti mmeshindwa hadi leo kujibu hoja, hamna vielelezo mnatafuta wapi kabati lipi ambalo hamjapekua na ni lipi mtapekua ili mpate majibu ndiyo maana nimeleta timu ya mkoa tusaidiane kupekua kwa pamoja ili tupate majibu kamili kwa hiyo fedha zote zenye mashaka kamati maalumu izifanyie kazi,” amesisitiza Mhandisi Gabriel.
Mhandisi Gabriel amehitimisha ziara yake ya Baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za CAG wilayani Ukerewe huku akiwa ameacha maagizo mbalimbali katika halmashauri zote ili kuhakikisha wanatekeleza hoja hizo likiwemo la kuwabaini wabadhilifu wa fedha za umma ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Maagizo mengine ni kubuni vyanzo vipya vya mapato lengo likiwa ni kuongeza mapato kwakuwa ni moyo wa halmashauri maana fedha hizo ndiyo zinazotekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwasaka watumishi waliolipwa fedha wakati wamestaafu ili warudishe fedha hizo kwa kuwa wako katika mfumo wa malipo ya mifuko ya hifadhi ya jamii na wana namba za hundi za malipo.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile, amewataka watumishi hasa wakuu wa idara kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kabla ya kutumia hata senti moja kwenye fedha za umma wafikirie hoja za CAG.