21.4 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yawataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuanzisha Klabu za UKIMWI

Na Ramadhan  Hassan, Dodoma

Serikali imewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zinazotekeleza mradi wa Timiza Malengo kusimamia kwa ufanisi mambo matatu ikiwemo kuanzisha na kuimarisha klabu za UKIMWI ambazo zitawezesha wanafunzi kujadili na kujifunza mada zilizowekwa katika vishikwambi.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Juni 28,2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vishikwambi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kwenye mradi wa timiza malengo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko akizungumza kwenye hafla hiyo.

Katika hafla hiyo, Simbachawene alimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na shule 36 za msingi na sekondari zilipatiwa vishkwambi hivyo.

Simbachawene amewaagiza Wakurugenzi hao kuanzisha na kuimarisha klabu za Ukimwi ambazo zitawezesha wanafunzi kujadili na kujifunza mada zilizowekwa katika vishikwambi.

Pia amewataka kusimamia na kufuatilia uwajibikaji wa Maafisa ugani katika kusimamia maendeleo ya mradi huo kwa walengwa na kuwawezesha kwenye mfumo wa wanawake,vijana na wenye ulemavu (4-4-2).

Vilevile, kusimamia matumizi sahihi ya zana kwa uendelevu wa mradi kwenye Halmashauri husika.

“Nichukue fursa hii kutoa rai kwa vijana wote nchini hasa walio katika eneo la mradi hususan wasichana ambao wanalengwa na mradi huu mfanye juhudi za kujikinga na maambukizi mapya ya VVU.

“Wale mliokoshuleni hakikisheni mnaweka mkazo katika elimu na kujiepusha na tabia zote  hatarishi  zinazopelekea kupata maambukizi ya VVU ili muweze kutimiza ndoto,” amesema Simbachawene.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema anaamini vishkwambi hiyo vitatumika vizuri kuongeza maarifa kwa wanafunzi pamoja na ufaulu.

“Sasa hivi vitabu vyote vinapatikana online sasa kupitia vishakwambi hivi naamini vitahusika kuwekwa pia programu za vitabu ili wanafunzi wajifunze kupitia Tehama,” amesema.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko amesema lengo la mradi wa timiza malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana ni kusaidia kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi wenye umri wa kuanzia miaka 10-24.

Amesema mradi huo unalenga kuwasaidia wasichana walio ndani ya nje ya shule kwa kuwajengea uwezo wa fikra, maarifa ili wakati wote wabaki salama dhidi ya maambukizi ya VVU na waweze kulijenga taifa imara.

Amesema mradi huo ni wa miaka mitatu na unatekelezwa katika mikoa mitano na Halmashauri 18 zikiwemo zile za Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Molel amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kuwaongezea ujuzi wanafunzi kupitia Tehama kwa ajili ya kizazi cha baadae kiweze kufanya mambo makubwa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, Dk. John Jingu amewataka walimu hao kuvitunza vishkwambi hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles