24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti ya CAG| Mashirika 14 ya kibiashara yanajiendesha kwa hasara

*ATCL yaendelea kupata hasara

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021 inaonesha Mashirika 14 ya kibiashara yanajiendesha kwa hasara likiwemo Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Akizungumza leo Aprili 12, 2022 jijini Dodoma na Waandishi wa Habari baada ya asubuhi kuiwasilisha ripoti hiyo bungeni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk. Charles Kichere amesema kwa miaka miwili 2019-2020 na 2020-2021 mashirika 14 ya kibiashara yalipata hasara mfululizo.

“Hali hiyo ilisababishwa na hasara kwenye uwekezaji uliofanywa, ufanisi duni wa mashirika husika na udhibiti hafifu wa mapato na matumizi,” amesema Kichere.

Amesema kampuni ya ATCL kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya Sh milioni 36,499.20 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara ya Sh milioni 60.

CAG amesema Kampuni ya Biotech Production kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya Sh milioni 14,779.56 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara ya Sh milioni 15,073.79.

Ameyataja makampuni mengine yaliyojiendesha kwa hasara ni Kampuni ya Mkulazi, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kiwanda cha Kimataifa cha bidhaa za ngozi Kilimanjaro,(KILC), Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Shirika la uuzaji bidhaa Tanzania (EPZA).

Pia, kampuni ya kuzalisha nguo za umeme za zege Tanzania (TCPM),Shirika la Posta Tanzania (TPC), Kampuni ya Nyumba za watumishi (Watumishi Housing), Kampuni ya T-PESA kampuni tanzu ya TTCL, Kampuni ya uwekezaji ya PPF, DCC, Kampuni ya uchapishaji ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (DUP) na Kampuni ya Umeme ya Kikuletwa.

CAG amesema hati za ukaguzi zinaonesha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kati ya hati 185 zinazoridhisha ni 178, zenye shaka sita, hati mbaya ni moja.

Amesema mashirika ya umma 195 yenye hati zinazoridhisha ni 185 zenye shaka nane hati mbaya hakuna na kushindwa kutoa maoni mawili.

Kwenye Serikali Kuu amesema hati kati ya hati 308 hati zinazoridhisha ni 305 zenye shaka mbili, hati mbaya moja na hakuna ambayo imeshindwa kutoa maoni.

Amesema Halmashauri zilizopata hati zenye mashaka ni ya Wilaya ya Kisarawe, Longido, Mlele, Musoma, Sengerema na Bunda.

Kwa upande wa mashirika ya umma ameyataja yenye hati zenye mashaka ni pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita, Taasisi ya Mifupa Muhimbili, Mamlaka ya Bandari Tanzania, kampuni ya magazeti ya Tanzania, shirika la mawasiliano Tanzania (TTCL).

Amesema kwa upande wa Serikali kuu, Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) imepata hati yenye mashaka pamoja na hesabu Jumuifu za Taifa huku Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) likipata hati mbaya.

Aidha, CAG amesema wakusanya mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 147 hawakuwasilisha benki makusanyo yanayofikia Sh bilioni 17.

Pia, mawakala wa kukusanya mapato katika mamkala za serikali za mitaa 12 hawakupeleka benki makusanyo ya Sh bilioni 3.31 kinyume na mikataba yao.

“Ninapendekeza kwamba Tamisemi iongeze usimamizi wa mapato na kuhakikisha makusanyo yanapelekwa benki bila kuchelewa,”amesema.

Vilevile, amesema mamlaka ya serikali za mitaa 24 zilitumia Sh milioni 664 katika matumizi yasiyo na manufaa kama vile malipo kwa riba na adhabu za kuchelewesha malipo na posho kwa watumishi wasiostahili.

Aidha, mamkala za serikali za mitaa 61 ziliagiza na kulipa sh bilioni 8.44 kwa ajili ya bidhaa ambazo hazikuwasilishwa  na wazabuni kwa muda wa hadi kufikia miezi 24.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles