Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii, imewapokea wachezaji 27 wa timu ya waendesha Baiskeli ya Twende Butiama pamoja na Wasanii wa Maigizo, jijini Dodoma ambao wataendesha baiskeli kwa zaidi ya Kilomita 1,500 mpaka Butiama mkoani Mara kwa ajili ya kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage.
Msafara huo umepokelewa leo Aprili 8, 2022 Makao Makuu ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Juma Mkomi na wafanyakazi wa wizara hiyo.
Mkuu wa msafara huo, Gabriel Landa amesema safari hiyo itakuwa ni ya siku tano na wameianza jana jijini Dar es Salaam na walilala Gairo na leo Aprili 8, wamefika jijini Dodoma na wanatarajia kulala Itigi mkoani Singida.
Amesema kesho safari yao Wataanzia Itigi mpaka Nzega na kisha Nzega mpaka Magu na watamalizia Magu mpaka Butiama.
“Safari kama hizi tumeanza tangu mwaka 2018 lengo ni kushirikiana na wizara katika kumuenzi Baba wa Taifa kwa kutimiza miaka 100 kama angekuwa hai. Nitoe shukrani kwa wizara kuendelea kuenzi yale mazuri ambayo yamefanywa na mwalimu Nyerere,”amesema.
Mkuu huyo wa msafara pia amesema wamekuwa wakihamasisha utalii ambapo wamewahi kwenda Ngorongoro, Mikumi na Kolo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkomi amesema kwao ni furaha kupokea timu hiyo ya waendesha baiskeli ambapo amewapongeza kwa moyo wao wa kujitoa kwa vitendo katika kuenzi mambo mazuri ambayo yamefanywa na Mwalimu Nyerere.
“Wametembea na baskeli kwa sababu wakati huo baiskeli ilikuwa ni muhimu na ilikuwa ikitumika kufikisha ujumbe. Wizara ya Maliasili na Utalii itaratibu zoezi hili mpaka kilele Aprili 13, Butiama.
Amesema wameamua kushiriki tukio la kuenzi yale yote ambayo ameyafanya na Baba wa Taifa kwasababu alikuwa ni muhifadhi namba moja wa vivutio vya Utalii nchini.
Kwa upande wake,Msanii wa Maigizo, Ahmed Olotu maarufu kwa jina la Mzee Chilo amesema kumuenzi Mwalimu Nyerere ni jambo muhimu kwani kuna baadhi ya vijana hawaelewi amelifanyia nini Taifa.
“Mataifa makubwa kama China wanawaenzi viongozi wao hata hapo Afrika Kusini na wao wanamuenzi Nelson Mandela kwanini isiwe sisi mimi na wenzangu tutaendelea kutangaza mazuri ambayo yamefanywa na Mwalimu Nyerere,” amesema.
Naye, Mwigizaji Korongo Hamis Maarufu Mzee Korongo amesema watamuenzi mwalimu Nyerere kwa kusema yale mazuri ambayo aliyafanya ili jamii iweze kujua.
Naye, Veronika Godfrey amesema atashindwa kumalizia mbio hizo kutokana na kupata maumivu ambapo amedai hiyo ni mara yake ya pili kushiriki huku akiwahamasisha wanawake kujitokeza kushiriki mchezo wa mbio za baiskeli.