NA SHABANI MATUTU
BUNGE la tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), linatarajiwa kufanyika kesho na kumalizika Septemba 5, mwaka huu katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia sababu za Bunge hilo kufanyia mkutano wake Dar es Salaam, Spika wa Bunge hilo, Dk. Margaret Zziwa, alisema umetokana na taratibu walizojiwekea za kufanya vikao kwa zamu katika nchi wanachama ili wajiweke karibu na wananchi kwa ajili ya kutambulisha shughuli zao.
“Ripoti hizo ni Kamati ya masuala ya Jumuiya na Upatanishi wa migogoro, kituo cha uongozi cha Afrika cha taasisi za Afrika Mashariki na Usalama wa Jumuiya, kamati ya kilimo, Utalii na Maliasili, semina ya wabunge wa jumuiya juu ya misitu na mabadiliko ya hali ya hewa na kamati ya mawasiliano, biashara, uwekezaji na usafiri wa sekta ya anga ya Afrika Mashariki,” alisema.
Dk. Zziwa alitaja miswada mingine iliyombele ya kamati za Bunge kuwa ni muswada wa elimu, muswada wa masuala ya ushirika na muswada wa masuala ya biashara.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Spika huyo alipata fursa ya kuzishukuru nchi wanachama kwa kuimarisha mchakato wa utengamano uliowezesha Umoja wa Forodha kuwa katika hatua nzuri ya utekelezaji.
Alitoa shukurani kwa Tanzania kutia saini kupitisha itifaki ya Umoja wa Fedha, ambako alisema utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mara baada ya nchi nyingine wanachama kuidhinisha itifaki hiyo na kukabidhi nyaraka hizo kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za Afrika Mashariki (EAC).
Naye Mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Shyrose Bhanji aliwatoa wasiwasi wananchi wa Afrika Mashariki kutokuwa na shaka na Spika wa bunge hilo kwa sababu mgogoro uliokuwa umetokea baina yake na wabunge umekwisha kwa taratibu za sheria za Bunge hilo.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa Bunge hilo kutumia Kiswahili, Bhanji alisema kuwa upo umuhimu wa kutumia lugha hiyo kutokana na kukubalika kutumika katika sheria za jumuiya hiyo.