*Asema michezo itaendelea kupewa kipaumbele nchini
Na Sarafina Sarwatt, Moshi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapiga hatua kwenda mbele kwani michezo ni zaidi ya burudani.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Februari 27, 2022) alipozungumza na wananchi wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Kilimanjaro Marathon 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MOCU). Ameshauri mbio hizo ziitwe Kilimanjaro International Marathon kwa kuwa zinashirikisha mataifa mengi duniani.
“Michezo hii inatusaidia katika kujenga afya, urafiki, kukuza ujasiriamali na kuimarisha sekta ya utalii. Michezo ni uchumi. Nimefahamishwa kuwa mbio hizi zimeshirikisha wakimbiaji zaidi ya 12,000 kutoka mataifa zaidi ya 55 duniani. Hii ni idadi kubwa sana na ni faida kubwa kwa nchi yetu kwani kupitia washiriki wa riadha hao kunawezesha nchi yetu kupata fedha za kigeni,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema mbali na kuimarisha hali ya uchumi, amesema michezo pia inaimarisha afya bora kwa kushiriki katika mazoezi au shughuli za nguvu kwa ajili ya kujikinga na maradhi ambayo yamekuwa yakiongeza gharama za matibabu na kupotea kwa nguvu kazi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii zishirikiane na waandaaji wa Kilimanjaro Marathon ili kutangaza zaidi fursa za utalii na vivutio mbalimbali kwa manufaa ya Taifa.
“Kilimanjaro Marathon ni chapa (Brand) kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo, nina hakika fursa zake zikitumika vizuri itasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini,” amesema Majaliwa.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipitie mitaala ya Elimu Msingi kwa ajili ya kufundisha elimu kwa michezo na kuanzisha vituo vya michezo (Sports Academy) ili watoto wenye vipawa waweze kulelewa na kukuza vipawa vyao.
“Hii itaiwezesha nchi yetu kuwa na wachezaji wenye utaalamu na mahiri ambao wataweza kuwakilisha vema Taifa letu kwenye medani za kimataifa. Suala hili lipewe kipaumbele kwani sote tunatambua kuwa michezo ni zaidi ya burudani na inao uwezo wa kutoa ajira ndani na nje ya nchi.
“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi zetu ione uwezekano wa kupatikana kwa fursa za kusomesha walimu wa michezo watakaosaidia kunoa timu zetu. Wakati umefika suala la michezo lichukuliwe uzito unaostahili kwani pamoja na mambo mengine michezo inao uwezo mkubwa wa kuinua pato la Taifa letu,’ amesema Majaliwa.
Amesema uwepo wa mchezo huo wa riadha ni fursa nzuri yakuendeleza utalii wa michezo yaani ‘sport tourism’.
“Washiriki wa mchezo huu pamoja na riadha wanapata fursa ya kufanya utalii katika vivutio vyetu mbalimbali kama vile Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na maeneo mengine,” amesema.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya cable cars zitakazotumika kupanda mlima Kilimanjaro, Waziri Mkuu amewataka wahusika wa mradi huo waandae mpango mkakati wa utekelezaji wake ambao utachambua athari za kimazingira pamoja na ajira hususani kwa vijana wengi wanaofanya shughuli za kiutalii kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amesema katika kusukuma mbele tasnia ya michezo, Serikai imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi na ushiriki wa timu za Taifa zikiwemo timu za riadha katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 1.5 zimetengwa.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya Michezo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha Sh bilioni 10.5 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Michezo (Sports Centres) katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Geita. “Vituo hivi vitakuwa ni kichochezo kikubwa kwa vijana wetu kushiriki katika michezo.”
Awali, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Marry Francis Masanja, amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kukuza utalii ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuifungua Tanzania kwa kuwezesha kupata masoko mapya ya utalii
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Breweries LTD, Jose Moran akiongea kwa niaba ya wadhamini wote wa Kilimanjaro Marathon ameihakikishia Serikali kwamba watahakikisha mbio hizo zinazidi kukua zaidi. Pia ameahidi kuendelea kudhamini mbio hizo ambazo wamekuwa wakizidhamini kwa muda wa miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.