MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, atakuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Changia Damu Okoa Maisha linalotarajiwa kuanza kesho katika Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Eligeisha, alisema Makamu wa Rais atashiriki kutoa damu Ijumaa, Februari 26, mwaka huu katika Uwanja wa Karume, jijini Dar pamoja na viongozi wengine.
“Lengo la tamasha hilo linaloitwa Changia Damu Okoa Maisha ni kukusanya lita kati ya 5,000 na 6,000 ambazo ni asilimia 75 ya mahitaji ya damu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.
Aliongeza kwamba, tamasha hilo kama linavyojieleza, damu itakayochangiwa itapelekwa benki ya damu kwa ajili ya wagonjwa watakaoihitaji.
Katika tamasha hilo pia wasanii mbalimbali watatumbuiza bure, wakiwemo Yamoto Band na wasanii kutoka THT.