Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri amesema atawazawadia wakuu wa shule watakaosimamia vyema ujenzi wa madarasa 255 ambayo yanatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Ujenzi wa madarasa hayo ni mpango wa Serikali kupitia mkopo wa Sh trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepata Sh bilioni 5.1 kujenga madarasa 255.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha wakuu wa shule, waratibu elimu kata na wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri hiyo Shauri amesema mshindi wa kwanza atapata Sh 500,000 wakati wa pili atapata Sh 300,000 na wa tatu Sh 200,000 na kwamba watapewa pia vikombe na vyeti.
“Tunataka jiji letu la Dar es Salaam liwe la mfano watu waje wajifunze hivyo kila mmoja jicho lake liwe kwenye fedha hizi, nisingependa mkuu wangu wa shule aadhibiwe kwa kazi hii tutamuangusha mheshimiwa rais…mkiona kuna ucheleweshaji wa aina yoyote au kuna mkuu wa idara anawakwamisha nijulisheni,” amesema Shauri.
Aidha ameziagiza kamati za ujenzi kutafuta mafundi wenye sifa na kuepuka kuwapa kazi mafundi wababaishaji huku akisisitiza kuwa kufikia Desemba 15 madarasa yote yawe yamekamilika.
“Nikikuta mlango mbovu nautoa kwa gharama za mkuu wa shule, najua darasa moja unatumia rangi kiasi gani hivyo, ukinidanganya najua,” amesema.
Naye Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwalimu Mussa Ally, amesema watahakikisha madarasa hayo yanajengwa kwa ubora na kukamilika haraka.
“Tumeingiziwa fedha nyingi hivyo tutegemee kufuatiliwa sana ndiyo maana tunaitana na kuelekezana, tunatarajia hatutakuwa na changamoto za ujenzi labda ziwe zile za kitendaji,” amesema Mwalimu Ally.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Elimu Kata ambaye pia ni Ofisa Elimu wa Kata ya Kariakoo, Rehema Gunda, amesema watashirikiana na kamati za ujenzi kusimamia madarasa hayo sambamba na miradi mingine inayotekelezwa kupitia mapato ya ndani kama vile mabweni na matundu ya vyoo.