28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah aweka wazi mikakati ujenzi barabara za lami kwenye mitaa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema fedha zitakazokuwa zikitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kila jimbo atazielekeza kwenye ujenzi wa barabara za lami katika mitaa kwa kuwa zinadumu kwa muda mrefu.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kipawa wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Karakata amesema Sh milioni 500 zilizotolewa mwaka huu zimeelekezwa kwenye ujenzi wa barabara ya Airport Karakata ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ni lango la Tanzania na nchi nyingine.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha hizi, tuna kata 13 tungeweza kuzigawanya kidogo kidogo lakini zisingefanya kitu kinachoonekana, tungesema kila diwani tumpe milioni 30 aweke kifusi mvua ikinyesha kunakuwa hakuna kitu,” amesema Bonnah.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akivuka katika kivuko cha muda kinachotumiwa na wakazi wa Kata ya Kipawa wakati wa kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Amesema Rais Samia amedhamiria kuboresha miundombinu hasa ya barabara hivyo watakuwa wakizitumia fedha hizo kujenga barabara za lami.

Aidha amesema kupitia mradi wa DMDP Mto Msimbazi utajengwa kingo ili wananchi waendelee kuishi na maji yaendelee kupita na kuwataka wananchi kutokuwa na hofu.

Naye Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, amesema kwa maeneo ambayo hayana miundombinu ya maji hivi sasa Dawasa inaendelea kutandaza mabomba katika Mtaa wa Mji mpya kisha Karakata, Uwanja wa Ndege na Stakishari ili kila mwananchi aweze kuunganishiwa maji.

“Dawasa wameondoa mikopo kwa sababu kuna wezetu walipata wamekuwa wasumbufu kulipa, kuna watu zaidi ya 20 wameunganishiwa maji na kufungiwa hadi mita halafu wanasema hawataki…hii ni moja ya sababu imetufanya tukose mikopo,” amesema Kwezi.

Aidha amesema madarasa 10 yamejengwa katika Shule ya Sekondari Minazi mirefu kwa gharama ya Sh milioni 200 wakati Sh milioni 14 zilizotolewa kupitia mfuko wa jimbo zimetumika kununua kompyuta katika shule hiyo na kujenga sehemu ya mapokezi katika Zahanati.

Amesema pia Shule ya Msingi Majani ya Chai imekarabatiwa kwa gharama ya Sh milioni 107 na kwamba hivi sasa ujenzi wa ukuta unaendelea wakati Shule ya Msingi Karakata zilitolewa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuikarabati.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akimsikiliza mmoja wa wananchi wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Kipawa.

Awali Meneja Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, Simon Mbaga, amesema tathmini kwa wakazi wa Uwanja wa Ndege wanaotakiwa kuhama kupisha mradi huo tayari imefanyika na wiki hii wataonyeshwa kila mmoja kiasi anachopaswa kulipwa.

“Tumejenga njia lakini hatutaweza kupitisha treni hadi tujenge barabara ya juu na madaraja kwahiyo Jumatano (kesho) mtasomewa kila mmoja kile ambacho amepangiwa kulipwa.

“Ukilipwa fidia hata kama eneo lako halitoguswa usiendeleze ujenzi, vunja ondoka kwa sababu kuna wengine walishawahi kulipwa kipindi cha nyuma na bado hawajaondoka,” amesema Mbaga.

Mmoja wa wakazi wa Karakata, Mary Mauki, ameomba eneo lake lifanyiwe tathmini upya kwa sababu iliyofanywa awali kuna eneo ambalo halikuguswa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles