Na Shomari Binda,Musoma
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amewapongeza, Mbunge wa Musoma Viijini, Profesa Sospeter Muhongo na yule wa Butiama, Jumanne Sagini, kwa ufatiliaji wa miradi ya maji kwenye majimbo yao.
Aweso ametoa kauli hiyo Septemba 16, 2021 wakati alipofanya ziara ya siku moja kutembelea mradi wa maji wa Mugango, Kiabakari na Butiama kwa ajili ya kuangalia utekelezaji wake.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu imekusudia kumtua Mama ndoo kichwani na wabunge hao wamekuwa mstari wa mbele kufanya ufatiliaji.
Aweso amesema fedha za mradi huo Sh bilioni 70 zipo jambo ambalo kwasasa usimamuzi mzuri unahitajika ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
“Niwashukuru sana waheshimiwa wabunge, kwa ufatiliaji wa miradi ya maji kwenye maeneo yao. Miradi ya maji ipo mingi hapa nchini na Mheshimiwa Rais Samia anataka ikamilike kwa wakati hivyo bila kuwa na wafatiliaji haitaweza kukamilika kwa wakati,” amesema Aweso.
Amesema serikali ipo tayari kuongeza Sh bilioni 3 kwenye mradi huo wa Mugango, ili bomba linapopita wananchi wa pembezoni waweze kupata maji.
Upande wake Prof. Muhongo, ameishukuru wizara ya maji kwa mradi huo, amesema ipo changamoto ya vijana kupewa ajira kwenye ujenzi wa mradi wanaotoka eneo hilo ambao wamekuwa wakilalamika kutokupewa ajira na kuomba kuangaliwa.