25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kidato cha nne mabingwa wapya Benjamini Mkapa Sekondari

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Timu ya mpira wa miguu ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa imeibuka mabingwa baada ya kuwasambaratisha timu ya kidato cha sita katika fainali ya ligi ya shule iliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo.

Mwanamitindo Flaviana Matata akikabidhi kikombe kwa nahodha wa timu ya soka ya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ambayo iliibuka mshindi katika fainali za ligi ya shule hiyo. Kulia ni Mkuu wa shule hiyo, Deo Joseph.

Mashindano hayo yaliyoanza Agosti 11 pia yalihusisha michezo ya riadha, rede, kukimbiza kuku, kukimbia kwa magunia na mpira wa miguu kwa wanawake.

Mwalimu wa Michezo katika shule hiyo Seleman Haji, amesema kulikuwa na timu sita kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ambapo michezo ilifanyika kwa mtindo wa makundi. Kundi A lilikuwa na kidato cha kwanza, tatu na tano wakati kundi B lilikuwa na kidato cha pili, nne na sita.

Aidha timu nne kutoka katika makundi hayo zilingia nusu fainali kisha zikapatikana timu mbili kidato cha nne na sita zilizocheza fainali.

“Lengo kubwa la ligi ni kupata vipaji ili tuweze kutengeneza timu ya shule ambayo itakuwa imara kuweza kupambana na shule nyingine na hilo limefanikiwa sana, kila mtu ameshuhudia vipaji vya kipekee na tunaamini tutakuwa na timu ya shule ambayo itatoa upinzani kwa shule nyingine,” amesema Mwalimu Haji.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa wakishangilia baada ya kunyakua ubingwa wa soka wakati wa fainali zilizofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo.

Naye Kaka Mkuu wa shule hiyo Hassan Ally, amesema kuna vipaji vingi na kupitia mashindano hayo vimeonekana.

Kwa upande wake Mwanamitindo Flaviana Matata ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hizo amewapongeza washindi na kuzitaka shule nyingine kuwa na mashindano kama hayo ili kuibua vipaji na kuviendeleza.

Flaviana ambaye alidhamini mashindano hayo kupitia kampuni yake la Lavy, alikabidhi kikombe na medali kwa washindi pamoja na taulo za kike kwa wasichana walioibuka washindi.

“Michezo ni sehemu muhimu ya masomo inasaidia kuchangamsha akili, kuibua vipaji na kwenye nchi zilizoendelea tunaona watoto wanapata ufadhili kutokana na vipaji vyao hivyo, tuendelee kuwapa hamasa na kuwaunga mkono vijana shuleni kupitia michezo,” amesema Flaviana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles