Na Clara Matimo, Mwanza
Katika kuhakikisha huduma ya mafuta ya taa, dizeli na petroli inatolewa kwenye maeneo salama na yanayokidhi vigezo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka wawekezaji katika sekta ya nishati kujenga vituo vya kutolea huduma hiyo(sheli) vyenye ubora.
Wito huo umetolewa Jumanne Agosti 31, na Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina, wakati akitoa elimu kwa washiriki wa maonesho ya 16 ya biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea kwenye viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza walioambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ambaye alitembelea banda hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel.
Amesema moja ya majukumu ya Ewura ni kupanga viwango vya ubora kwa kushirikianana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hivyo wanaendelea kuwahimiza wawekezaji katika sekta ya nishati kutumia gharama ndogo lakini ambazo zitakuwa na matokeo yenye ubora katika kujenga sheli zao.
“Naamini pamoja na wajumbe wote ulioambatana nao kwenye banda letu mtakubaliana na mimi kwamba vituo vya kutolea huduma ya mafuta vya zamani ni tofauti kabisa na vya siku hizi, hata ubora wa mafuta yanayoingia nchini ni tofauti na zamani.
“Hii inatokana na usimamizi madhubuti ambao tunaufanya ewura kwa kushirikiana na TBS hivyo kupitia maonesho haya nazidi kuwasisitiza wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya nishati wafike katika banda letu ili tuwape elimu zaidi watakapojenga vituo view vinavyokidhi vigezo vyote vya ubora ambavyo tunavitaka,” alisema Mhina.
Mhina ametaja majukumu ya Ewura kuwa ni pamoja na kutoa leseni za wafanyabiashara wa nishati na mafuta, kupanga bei za umeme na maji, kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya watoa huduma hizo.
“Bei za umeme na maji tunazipanga kila baada ya miaka mitatu lakini mafuta tunabadilisha bei kila jumatano ya kwanza ya mwezi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazotuongoza za ewura,”alisema.
Kwa upande wake Makilagi ambaye alikuwa mgeni rasmi na kufungua maonesho hayo, aliipongeza ewura kwa kuhimiza wawekezaji kujenga vituo vya kutolea huduma ya mafuta vyenye gharama nafuu.
Maonesho hayo huratibiwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza lengo likiwa ni kukuza masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kukutanisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuinua uchumi wa nchi na wafanyabiashara wa ngazi zote.