27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tundu Lissu ajisalimisha polisi

tundu lissuNa Asifiwe George, Dar es Salaam

MBUNGE Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), jana alijisalimisha polisi na kuhojiwa zaidi ya saa moja kuhusu habari iliyosababisha kufutwa kwa gazeti la Mawio kwenye daftari la Msajili.

Akizungumza  Dar es Salaam jana baada ya mahojiano na   polisi, Lissu alisema alifika kituoni hapo baada ya kupokea wito kutoka kwa maofisa wa jeshi hilo kumtaka ajisalimishe Kituo Kikuu cha  Polisi.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema alifika kituoni hapo saa 4:00 asubuhi akiwa amefuatana  na mawakili wake watatu, Peter Kibatala, Fredeli Kihwelo na Hekima Mwasibu.

Mawakili hao pamoja na mteja wao walikaa kwa muda mrefu kituoni hapo bila kuambiwa chochote kabla ya  kuwauliza maofisa wa polisi sababu za wito huo.

Lissu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi walimwambia aliitwa kituoni hapo kama mtuhumiwa wa uchochezi  baada ya kufanyiwa mahojiano na gazeti la Mawio  na kunukuliwa katika  habari iliyopewa kichwa cha habari kwamba  ‘haki isipotendeka Zanzibar  upo uwezekano wa kumwaga damu’, habari ambayo ilisababisha gazeti hilo kufutwa.

“Rais Magufuli amevalishwa mzigo wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete hivyo kwa sababu yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu anahusika moja kwa moja hivyo suluhisho la  siasa  Zanzibar lisipopatikana Rais wetu anaweza kuburuzwa katika Mahakama za kimataifa (ICC).

“Waliofuta uchaguzi Zanzibar  walitumia nguvu za  jeshi, sasa polisi nao wanataka kutumia nguvu  za kutuziba midomo …bado ninaendelea kusisitiza kuwa suluhisho la Zanzibar  lisipopatikana upo uwezekano wa kumwaga damu hivyo hatutakubali kuzibwa midomo kuhusu uchaguzi wa Zanzibar,” alisema Lissu jana.

Lissu alisema baada ya kumaliza mahojiano na polisi alielezwa kuwa jalada lenye maelezo yake litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na endapo atahitajika atapewa taarifa.

Alisema miaka 15 iliyopita  polisi waliwahi  kumuhoji kwa   saa sita kuhusu mgogoro wa madini  kati yake na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles