Na Derick Milton, Bariadi
Mbunge wa Jimbo la Bariadi na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknologia ya Habari, Andrew Kundo amelitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mkoa wa Simiyu kuondoa nyaya ambazo zimepita juu ya nyumba za wananchi.
Kundo ametoa agizo hilo leo Jumamosi Agosti 28, wakati wa mkutano wake wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Mwamlapa kata ya Sapiwi Jimboni humo, mara baada ya kupokea malalamiko toka kwao juu ya nyaya za umeme kupitishwa juu ya nyumba zao.
Kabla ya kutoa agizo hilo, baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho walimweleza Mbunge huyo kuwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa REA katika Kijiji chao walishangaa kuona Tanesco wakipitisha nyaya juu ya nyumba zao.
Wamesema kupitisha nyaya juu ya nyumba zao bila ya hata wao kupewa taarifa ni kinyume cha utaratibu, ambapo walimtaka mbunge huyo kuwatatulia kero hiyo kwani inawazuia kufanya maendeleo na ni hatari kwao na familia zao.
“Tunaomba kusaidiwa baadhi yetu, nyumba zetu zimepitiwa na nyanya za umeme juu, wakati wa utekelezaji wa mradi wa REA mafundi wakapitisha nyanya juu ya nyumba zetu, tunaomba kusaidiwa,” ameeleza Oscar Charles, Mwananchi.
Kabla ya kutoa maagizo mbunge huyo aliamua kwenda kuangalia nyumba hizo, ambapo alikuta ni kweli nyaya zimepita juu ya nyumba za wananchi hao kama walivyolalamika.
Mbunge huyo alilitaka Shirika hilo kumwelekeza mkandarasi ambaye alikuwa anatekeleza mradi huo katika Kijiji hicho kuondoa nyanya zote ambazo zimepita juu ya nyumba za wananchi wake.
“Hawa wakienda kuwashtaki wanawashinda na mtawalipa pesa nyingi, kisheria ni kosa kupitisha nyanya juu ya nyumba ya mtu, niwaombe Tanesco hizo nyaya ziondolewe maana siyo sahihi na ni hatari kwa wananchi,” amesema Kundo.
Akiongea kwa niaba ya Meneja wa Tanesco mkoa, Ofisa mahusiano wa Shirika hilo mkoa Ben Kirumba amekiri kuwa kupitisha nyaya ni kosa na hairuhusiwi hivyo nyanya hizo zitaondolewa.
“Mradi huu ulikuwa unatekelezwa na mkandarasi White City, Kwanza niseme ni kosa kupitisha nyaya juu ya nyumba, tutamwelekeza mkandarasi aje aziondoe,” amesema Kirumba.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo ametoa mabati 300 kwa ajili ya shule ya Sekondari Mwamlapa kukamilisha ujenzi wa maabara pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa jengo moja katika zahanati ya Kijiji hicho.