IKULU ya Magogoni imetoa taarifa ndefu inayoelezea mafanikio ya utendaji kazi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, katika kipindi cha siku 100 alizokaa madarakani.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ikiwa ni siku moja baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu mwenendo wa utendaji kazi wa Rais Magufuli kwa muda wa siku 100 akiwa katika ofisi yake mpya ya Ikulu ya Magogoni.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Rais Magufuli amefanikiwa kutekeleza kwa ufanisi yale ambayo yaliyoshindikana kwa muda mrefu.
Alisema mambo yaliyosimamiwa na Rais Magufuli kwa ufanisi mkubwa ni pamoja na kufutwa kwa sherehe za Uhuru na badala yake kufanya usafi nchi nzima ili kupambana na magonjwa ya kuambukiza na fedha zilizolengwa kugharamia sherehe hizo kutumika kujenga sehemu ya barabara ya Bagamoyo kutoka Mwenge hadi Morocco.
Sefue alitaja jambo jingine kuwa ni kufutwa kwa sherehe za wabunge kujipongeza na fedha za sherehe hizo kuelekezwa kwenye ununuzi wa vitanda vya wagonjwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mambo mengine aliyoyataja ni kufutwa kwa sherehe za Siku ya Ukimwi na kuelekeza fedha hizo kununua dawa za kufubaisha makali ya ugonjwa huo.
“Badala ya semina elekezi ya mawaziri, fedha zake zitakwenda kutekeleza mradi wa kufunga vifaa vya kisasa vya kuchunguza magonjwa katika hospitali 37 kote nchini.
“Badala ya safari za nje fedha zilizookolewa zitatumika kwenye miradi ya maendeleo. Zaidi ya Sh bilioni 7 ambazo zingeweza kutumika kwa safari za nje zimeokolewa katika siku 100 na zitatumika kwenye miradi hiyo ya maendeleo,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia Rais Magufuli kutofanya safari za nje alisema uamuzi wake huo unalenga kulinda sifa ya nchi kwa kunyoosha kwanza mambo ndani ya nchi.
“Tofauti na wanaomlaumu Rais kwa kutosafiri nje ya nchi, anafahamu na anawashukuru marais waliomtangulia kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga uhusiano mzuri na nchi za nje.
“Lakini Rais anatambua kuwa ili ailinde sifa hiyo na kuikuza, lazima anyooshe mambo kadhaa ndani ya nchi. Iwapo Tanzania itabaki kuwa masikini, yenye rushwa, ujangili, dawa za kulevya na kadhalika, hiyo sifa nzuri nje ya nchi itaporomoka.
“Hivyo ameamua kujipa muda kuimarisha uchumi na maendeleo ndani ya nchi kwa kupambana na matatizo mengine yanayoharibu sifa yetu ili iwe rahisi kudumisha sifa ya Tanzania nje ya nchi,” alisema Sefue.
Kuhusu mapato, Balozi Sefue alisema kwa siku 100 za kwanza Serikali imefanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi hadi kufikia Sh trilioni 3.34, ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 2.59 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2014/15, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 746.31.
“Kwa mapato yasiyo na kodi, makusanyo yameongezeka hadi kufikia Sh bilioni 281.68, kutoka Sh bilioni 224.03 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2014/15, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 57.65.
Alisema ukusanyaji huo wa mapato umeiwezesha Serikali kugharamia baadhi ya miradi yake kwa fedha za ndani, mathalani, kuwalipa wakandarasi, kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji, miundombinu, umeme, kilimo, uwezeshaji wa vijana na kadhalika.
“Rais amethibitisha nia yake ya kutoa fursa sawa kwa sekta binafsi. Ameonesha kuwa wenye fedha wasiwe na kiburi cha fedha wakifikiri wana leseni ya kufanya watakavyo au kuonea wengine.
“Wahenga walisema nyota njema huonekana asubuhi. Naam! Katika siku 100 za kwanza, Rais Magufuli amethibitisha kwa uwazi zaidi kuwa yeye ni kiongozi bora na wa kupigiwa mfano.
“Kiongozi bora lazima awe na mikakati ya kutekeleza dira na maono yake pamoja na kufikia malengo katika vipindi tofauti. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli amedhihirisha anayo sifa hiyo. Kiongozi bora lazima aheshimike na awe na mvuto wa kuwafanya wananchi wamwamini na kumfuata. Rais amewafanya hata ambao hawakumpigia kura wamwamini, wamwombee na kumfuata,” alisema Balozi Sefue.
Kuhusu utendaji wa Serikali, Balozi Sefue alisema Rais amebadili utendaji wa Serikali kwa kupunguza urasimu, kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wenye masilahi kwa Taifa hususani katika sekta ya viwanda.
“Amebana matumizi kwa kupunguza yale ambayo kwa kuzingatia hali yetu ya uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika. Ameimarisha huduma za jamii hasa maeneo yenye kero zaidi kwa wananchi, amehimiza na kusimamia utii wa sheria, kurejesha nidhamu ya Serikali na uzingatiwaji wa maadili kwa viongozi wa umma na watumishi wa Serikali, sekta binafsi na watu wote kwa ujumla,” alisema Sefue.
Alisema Rais amedumisha ulinzi na usalama na kuendeleza uhusiano mzuri na wenye tija baina ya Tanzania na nchi za nje, mashirika na taasisi za kikanda na kimataifa pamoja na wabia wengine wa maendeleo.
Kuhusu nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu, alisema katika siku hizi 100 za kwanza, Rais ametekeleza majukumu yake kwa wepesi na uhodari.
“Amekuwa karibu na Jeshi na viongozi wake. Amekagua vifaa vya Jeshi na mazoezi ya kijeshi. Ameteua viongozi wa Jeshi na kutoa kamisheni kwa maofisa wapya. Ametoa maelekezo mahususi ya kuimarisha Jeshi na utendaji wake,” alisema Sefue.
Aligusia pia sifa binafsi za Rais Magufuli kwa kueleza kuwa ni mkweli.
“Wapo watu wanaofikiri kuwa siasa ni ujanja na ulaghai. Rais wetu amethibitisha kuwa yeye si mwanasiasa wa aina hiyo,” alisema.
Alitaja pia utekelezaji wa ahadi huku akitoa mifano ya kupunguza ukubwa wa Serikali kwa kupunguza idadi ya mawaziri na naibu mawaziri kutoka 55 hadi 35, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu kutoka 56 hadi 50 na elimu bure kutoka elimu ya msingi mpaka kidato cha nne.
“Alipoiahidi Mahakama kuwa atawapa fedha zao zote za maendeleo, Sh bilioni 12.3 ndani ya siku tano ametekeleza hata kabla siku hizo hazijaisha,” alisema Sefue.
Alitaja pia urejeshwaji wa miliki ya Serikali, kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo mkoani Tanga ambacho kilikuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu.
Kuhusu sifa ya usimamizi wa nidhamu bila woga akitoa mfano wa orodha ni kubwa ya viongozi na watumishi waliochukuliwa hatua mbalimbali za kisheria na kinidhamu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
“Tumedhamiria kurejesha nidhamu ya kazi na kutokomeza utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha. Katika tafsiri pana zaidi, hatua hizo zinalenga kukuza utamaduni wa uadilifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa uhodari, bidii na ufanisi mkubwa, kunakoendana na kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’,” alisema Balozi Sefue.