VIGOGO 11 wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, wamewapandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka kwa kuingizwa nchini mabehewa 25 ya kokoto yasiyokuwa na vigezo.
Washitakiwa wengine ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiraga, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomwiles, Mhandisi Mkuu, Mathias Massae, Kaimu Mhandisi Mkuu, Muungano Kaupunda.
Pia wamo Mhandisi Mkuu, Paschal Mfikiri, Mhandisi wa Karakana, Kedmon Mapunda, Kaimu Mhandisi wa Mawasiliano, Felix Kashaigili, Mkuu wa Usafirishaji wa Reli, Lowland Simtengu, Mkuu wa Michoro, Joseph Syaizyagi na Kaimu Meneja Mkuu wa Usafirishaji, Charles Ndenge.
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru na kusomewa mashitaka tisa ya matumizi mabaya ya madaraka na kutumia nyaraka za uongo kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao.
Wakati wakisomewa mashitaka, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theophil Mutakyawa na waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Max Ali na Maghela Ndimbo.
Kisamfu anadaiwa tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2013 na Juni 30, mwaka juzi katika makao makuu ya TRL, akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji kwa nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kusimamia mkataba wa zabuni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 kama ilivyotakiwa katika vigezo na masharti yaliyotajwa wakati wa utoaji wa mkataba, hivyo kwenda kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma na kusababisha Kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industries Limited kujipatia manufaa kutoka katika mkataba huo.
Mafikiri anadaiwa tarehe tofauti kati ya Julai Mosi na Agosti 31, 2013, katika ofisi hizo kwa nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kuidhinisha michoro ya mabehewa hayo ya Ballast Hopper Wagon iliyoandaliwa na kampuni hiyo ya India kinyume na vigezo na masharti ya mkataba huo na bila ya kuhakikiwa na kitengo cha kubuni hivyo kuipa manufaa.
Kisiraga na Massae wanadaiwa kuwa Agosti 5, mwaka juzi katika ofisi hizo walitumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha malipo ya dola 1,280,593.75 za Marekani kupitia barua ya malipo, kulipwa kampuni hiyo bila ya kujiridhisha kama mabehewa yamejaribiwa na kuonekana yanafaa na kutolewa vyeti na TRL iwapo yanafanya kazi kwa muda waliopewa wa miaka miwili.
Kaupunda anadaiwa kati ya Januari Mosi na Februari 28, mwaka jana katika ofisi hizo walitumia madaraka yao vibaya kwa kuridhika kwamba kampuni hiyo kutengeneza mabehewa hayo bila kujiridhisha na vigezo na masharti yaliyokuwepo katika mkataba.
Shitaka la tano linamkabili Ngosomwiles anayedaiwa tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi na Mei 31, mwaka juzi katika ofisi hizo alitumia madaraka yake vibaya kwa kuidhinisha kampuni hiyo kutengeneza mabehewa hayo bila ya kujiridhisha kwamba yatatengenezwa kwa kufuata maelekezo na vigezo vilivyoko katika mkataba.
Kaupunda, Mapunda, Kashaigili na Simtengu wanadaiwa kati ya Januari Mosi na Februari 28, 2013 wakiwa wajumbe wa kamati ya tathimini ya zabuni, walitumia madaraka yao vibaya kwa kupendekeza kampuni hiyo inastahili kupata zabuni wakati ikiwa haina sifa.
Washitakiwa Kisiraga na Ndenge wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Februari Mosi na Machi 31, mwaka juzi walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha kufunguliwa kwa mahali ambako fedha hizo zitawekwa benki kabla ya kupokea na kuisha kwa muda wa miaka miwili ulioelezwa katika vigezo na masharti ya mkataba.
Kaupunda anadaiwa kati ya Januari Mosi na Februari 28, mwaka juzi kwa nia ya kumdanganya mwajiri wake ambaye ni TRL huku akijua alitumia taarifa ya ukaguzi wa behewa la mfano ya Januari 20, mwaka jana iliyokuwa na taarifa za uongo kwamba mabehewa hayo yametengenezwa kwa mujibu wa matakwa ya mkataba.
Shitaka la tisa linamkabili Ngosomwiles anayedaiwa tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi na Mei 31, mwaka jana kwa nia ya udanganyifu alimdanganya mwajiri wake kwa kutumia taarifa ya ukaguzi kabla ya mabehewa kusafirisha kutoka India kuja nchini yalitengenezwa kama ilivyokusudiwa wakati akijua ilikuwa na taarifa za uongo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka na Wakili Kimaro alidai upelelezi haujakamilika na hawana pingamizi na dhamana kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yanadhaminika.
Hakimu Mchauru alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka kila mshitakiwa kutia saini dhamana ya Sh milioni 10 na kuwa na wadhamini watatu kutoka serikalini au taasisi zinazotambuliwa ambao nao kila mmoja atatia saini kiasi hicho cha dhamana.
Pia kwa wale washitakiwa watakaotimiza masharti ya dhamana hawataruhusiwa kutoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama. Washitakiwa Massae, Kaupunda na Ndenge walitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa na kesi imepangwa kutajwa Februari 25, mwaka huu.