29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 29 kumaliza tatizo la maji Mji wa Malampaka

Na Samwel Mwanga,Simiyu

ILI kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mji wa Malampaka ulioko katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kiasi cha Sh bilioni 29 kinahitajika.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa), Mhandisi Nandi Mathias wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Alhamisi Julai 22, 2021 waliotembelea mji huo kuona changamoto ya hali ya upatikanaji wa maji.

Amesema mji huo ni moja ya maeneo mapya ya Mamlaka hiyo yaliyoongezwa ili kuyahudumia kwani awali eneo hilo lilikuwa likihudumiwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa mazingira Vijijini( Ruwasa) wilaya ya Maswa kwa lengo la kuboresha huduma ya maji katika mji wa Malampaka.

“Malampaka ni eneo jipya la huduma  ya maji ambalo imeongezwa kutoka Ruwasa lengo kubwa kuletwa huku Mauwasa ni kuboresha huduma ya maji katika mji huo kutokana na kuwa na shughuli nyingi za uchumi.

“Waziri wa Maji kwa mamlaka aliyonayo kwa kutumia sheria na 5 ya mwaka 2019 aliamua kuongeza eneo la huduma katika mji ya Lalago, Sangamwalugesha na Malampaka ambayo sisi Mauwasa tunaihudumia kwa sasa,” amesema Mhandisi Mathias.

Mhandisi Mathias amesema baada ya kukabidhiwa rasmi Mauwasa kutoa huduma maji katika miji hiyo walipitia hali ya upatikanaji wa maji na kubaini kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu hivyo kuamua kuandika andiko kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika miji hiyo mpya.

Amesema kwa mji wa Malampaka walibaini kuwa kuwa ina idadi ya zaidi ya wakazi 15,000 na mahitaji yao ya maji ni lita Milioni moja kwa siku ila uzalishaji kwa sasa ni lita 100,000 kwa siku hivyo hayatoshelezi hivyo wameshachukua ya kuandika andiko wizarani ili wapatiwe kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.

“Tayari andiko limewasilishwa wizarani kwa hatua za maamuzi zaidi  kwani tumeomba kiasi cha Sh bilion 29 ambazo zinahitaji ili kupata maji kutoka kwenye chanzo cha Ziwa Victoria ambacho kinatumiwa na KASHWASA na kitanufaisha zaidi ya wakazi wapatao 45,656 katika mji wa Malampaka pamoja na vijiji vya Mwakulwe na Kata ya Mwakilyambiti katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza,” amesema Mhandis Mathias.

Aidha, amesema kwa sasa wameweza kuwaunganisha wateja 235 ambao wanapata maji majumbani pia wana vituo 15 vya kuchotea maji ambapo kwa ndoo ya lita 20 huuzwa kwa Sh 50.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Malampaka wamesema kuwa pamoja na changamoto ya upatikanaji wa maji kutotosheleza kutokana na mahitaji yao lakini kuwepo kwa maji hayo kumewapunguzia umbali wa kufuata maji.

“Maji kweli hayatoshelezi lakini kwa haya tunayoyapata yanatusaidia sana maana kipindi cha nyuma tulikuwa tunatumia umbali mrefu kufuata maji kwenye mto na visima vya kuchimba pembeni mwa mto ambayo si safi na salama,”amesema Mariam Khija.

Pia wameiomba serikali kuharakisha kukamilisha mradi huo wa maji kutoka Ziwa Victoria kwani kwa sasa mji huo umekuwa na idadi kubwa ya watu kufuatia kuanza kwa ujenzi wa Bandari kavu katika reli ya kisasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles