23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Apewa mtoto mmoja akidai alijifungua watoto wawili mapacha

Na Mwandishi wetu Simiyu

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mwanamke mmoja, Zawadi Sayi Abdallah, mkazi wa Kidinda Halmashauri ya Mji wa Bariadi, amewalalamikia wahudumu wa afya katika hospitali ya halmashauri hiyo (Somanda) kumpatia mtoto mmoja badala ya wawili (mapacha) aliojifungua.

Tukio hilo la kustahajabisha, linadaiwa kutokea Mei 23, 2021 baada ya Zawadi kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua huku akiwa ameambatana na Mama yake mzazi Joyce Lujiga ambaye alikuwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari nyumbani kwao, Zawadi pamoja na mama yake wamesema kuwa walishangaa pia kuona wanatakiwa kugharamikia vifaa tiba na dawa ambavyo vilihitajika kwenye zoezi la upasuaji.

Kwa mujibu wa Zawadi, siku hiyo baada ya kufika hospitalini hapo saa za mchana, alipimwa na madaktari (majina tunayahifadhi) na kumwambia kuwa ana watoto mapacha hivyo anatakiwa kufanyiwa upasuaji.

“Baada ya majibu hayo ya vipimo, walimweleza mama yangu (Joyce) kuwa anatakiwa kusaini fomu za kwenda kufanyiwa upasuaji, naye mama akawasiliana na Baba yangu na Mume wangu wakaruhusu ndipo nikapelekwa chumba cha upasuaji,” aamesema Zawadi.

Aidha, mama Joyce ambaye ni mama yake zawadi amefafanua kuwa, baada ya zoezi la upasuaji kwenda vyema huku mtoto wake Zawadi akiwa hajitambui, alishangaa kuona analetewa mtoto mmoja wa kiume badala ya mapacha kama ambavyo waliambiwa mwanzo.

“Kwa kuwa mwanangu (Zawadi) alikuwa hajitambui kufutaia upasuaji na dawa za usingizi, niliona wananiletea mtoto mmoja, nikashangaa, nikawauliza mtoto mwingine yuko wapi?…

“Daktari huyo huyo aliyetupima mwanzo, akasema mtoto ni mmoja huyo tu…hakuna mwingine bali alikuwa mkubwa kilo nne, nikabaki nashangaa na Zawadi baada ya fahamu kurejea akashangaa anapewa mtoto mmoja,” amesema Joyce.

Baada ya majibu hayo Zawadi na mama yake Joyce akiwa na mtoto wake mmoja wa kiume walirusiwa kwenda nyumbani na kuwaeleza wanafamilia na kuamua kukaa kimya kwani walifikiri majibu ya madaktari yalikuwa sahihi.

Hata hivyo siku chache baadae walipata taarifa mpya zilizowashtua.

“Baada ya wiki mbili kupita, nilirudi hospitalini hapo kwa ajili ya kusafishwa kidonda, ndipo nilipokutana na Mkunga mmoja jina lake silijui baada ya kuniona nikiwa nimekaa kwenye benchi nasubiri huduma huku nikiwa nimebeba mtoto wangu, aliniuliza kuwa mbona nimebeba mtoto mmoja, mwingine yuko wapi?

“Bila kujua nilimkatalia nikamwambia; “labda unanifananisha“, akasema wewe si unaitwa Zawadi…nikamwambia ndiyo, akasema yeye alikuwepo wakati wa upasuaji nilijifungua watoto wawili, nikabaki nashangaa kisha akaondoka,” anaeleza Zawadi.

Zawadi anasema mara baada ya kauli hiyo ya mkunga alikwenda moja kwa moja kwa mama yake na familia ili kuwaeleza alichokutana nacho jambo lilomshangaza kila mmoja aliyekuwa kwenye kikao hicho.

“Hivyo hapo ilibidi nirejee majibu ya daktari ndipo nilipobainikuwa yalikuwa ya uongo na majibu ya vipimo yalikuwa sahihi kwamba nilikuwa na watoto pacha,” amesema.

Mama yake Zawadi (Joyce) anasema kuwa baada ya kuletewa taarifa mpya na mwanae huyo, aliamua kwenda hospitali kueleza taarifa hizo kama zina ukweli na apate majibu mtoto yuko wapi.

“Nilifika kwa viongozi wa hospitali nilichokutana nacho ni majibu ya kejeli tu, wahudumu wote ambao walihusika kwenye upasuaji waliitwa lakini walianza kunishambulia kwa maneno ya kejeli…nikawauliza mtoto yuko wapi hawakunijibu nikaamua kuondoka,” aamesema Joyce.

Amesema baada ya kutopata majibu aliamua kurejea nyumbani na kukaa kimya huku wakitafakari wapi wanaweza kwenda kwa ajili ya kupata haki yao.

Gharama wakati wa kujifungua

Mbali na lalamiko hilo Mama yake Zawadi (Joyce) anasema kuwa kabla ya zoezi la upasuaji alipatiwa orodha ya vifaa na Daktari vinavyohitajika wakati wa upasuaji na kuelezwa anatakiwa kwenda nje ya hospitali kwenye maduka ya dawa muhimu kununua vifaa hivyo.

“Orodha ilikuwa ndefu sana, nilipokea karatasi hiyo nikaenda kwenye duka la hospitali wakanitajia gharama za vifaa vyote zikawa kubwa zaidi ya Sh 150,000 ndipo nikatoka nje ya hospitali nikanunua vifaa hivyo kwa Sh 130,000,” amesema Joyce.

Akionyesha stakabadhi yenye orodha ya vifaa hivyo pamoja na dawa, ilionekana kuwa na vifaa mbalimbali ikiwemo maji tiba (drip) pamoja na plastiki za kuvaa mikononi (glaves).

Uongozi wa Hospitali.

Alipotafutwa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Said Mlowosha kujibu tuhuma hizo, alikiri ofisi yake kupokea malalamiko ya Mwanamke huyo huku akibainisha kuwa ni kweli alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua.

Dk. Mlowosha ameeleza kuwa katika uchunguzi wa awali ambao wameufanya kukagua taarifa zake kwenye mafaili kuanzia alipopimwa hadi chumba cha upasuaji zilizoonyesha kuwa hakuna sehemu ambayo iliandikwa kuwa ana mapacha.

“Taarifa zote kwenye mafaili yake zinaonyesha alikuwa na mtoto mmoja ambaye alikuwa mkubwa uzito wa kilo 3.3, lakini tunaendelea na uchunguzi zaidi kubaini ukweli juu ya majibu na hicho kilichotokea,” amesema Dk. Mlowosha.

Aidha, ameongeza kuwa kuwa uchunguzi wa kina ambao unaendelea ni kubaini Muuguzi aliyemwambia Zawadi wakati aliporejea hospitalini hapo kwa ajili kusafishwa kidonda ili kuweza kujua kama ni kweli au hapana.

Mbali na hayo, Dk. Mlowosha amezungumzia suala la mteja huyo kutakiwa kununua vifaa vyote vya upasuaji, ambapo amesema sera inaeleza kuwa huduma kwa mama wajawazito ni bure hivyo nalo wanalifanyia uchunguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles