25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rais wa Z’bar avutia washiriki NMB 5K Run 2021

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameongoza mamia ya wakimbiaji walioshiriki mbio za kilomita 5 za ‘NMB 5K Run 2021,’ zilizodhaminiwa na Benki ya NMB, ambapo ushiriki wake uliwavutia wengi zaidi miongoni mwa waliojitosa katika Zanzibar International Marathon 2021

NMB 5K Run 2021 zilikuwa ni sehemu ya Zanzibar International Marathon – mbio zilizofanyika chini ya kaulimbiu ya ‘Tunakuza Uchumi wa Bluu Kupitia Michezo Zanzibar, zilizoanzia Ngome Kongwe na kuishia Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, ambako Dk. Mwinyi alikuwa mmoja wa waliokimbia kilomita 5.

NMB ilidhamini kilomita 5 kwa Sh milioni 35, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar katika kuhamasisha na kukuza utalii, kukuza Uchumi wa Bluu na kuchagiza jamii kudumisha utamaduni chanya wa kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukizwa.

Akizungumza kabla ya kukabidhi medali na zawadi kwa washindi wa kilomita 5, 10, 21, watoto, walemavu na wagonjwa wa afya ya akili walioshiriki mbio hizo, Rais Mwinyi aliwashukuru waratibu, lakini akawapongeza wadhamini, wakiwamo NMB kwa kuzirejesha mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya mwisho miaka 10 iliyopita.

Alisema waratibu na wadhamini wameonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na Serikali yake katika kukuza uchumi, kuhamasisha utalii na kuhimiza mazoezi ya viungo, huku akiitaja marathon hiyo kama chachu ya uibuaji na uendelezaji wa vipaji vya riadha vitakavyoitangaza Zanzibar kimataifa.

“Serikali inaahidi kuwa mashindano haya yatafanyika kila mwaka kuanzia sasa, ili Zanzibar iweze kupata wakimbiaji mahiri, huku tukiyatumia kama chachu ya kuhamasisha kukuza Uchumi wa Bluu, utalii na kuimarisha afya. Wito wangu kwa wadau ni kuanzisha mbio nyingi zaidi na kudhamini pia michezo mingine,” alisisitiza Rais Mwinyi.

Kwa upande wake, Benedicto Baragomwa, ambaye ni Kaimu Afisa Mkuu Ukaguzi wa Ndani wa NMB, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa mdhamini, na kwamba kutokana na NMB kuwa mdau Mkubwa wa maendeleo, haikuwa ngumu kwao kufanya uamuzi wa kujitosa Zanzibar International Marathon.

“Sisi Ni wadau wa maendeleo, na tukavutiwa na malengo ya uwepo wa mashindano haya, tukakubali kudhamini ili kuwa sehemu ya washiriki wa mchakato wa kukuza Uchumi wa Bluu, utalii na kuimarisha afya za Wazanzibar kupitia michezo.

“NMB tunaahidi kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila hatua inayolenga kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa,” alisema Baragomwa, ambaye alikimbia mbio za kilomita 5 sambamba na Dk. Mwinyi.

Aidha, Inyasi Nicodemus wa Arusha aliibuka mshindi wa kwanza wa NMB 5K Run 2021 upande wa wanaume, akifuatiwa na Sylvester Naali na Emmanuel Gadiye (wote wa Polisi), huku kinara upande wa wanawake akiwa ni Aisha Luvuma wa Arusha akifuatiwa na Valentina Michael (Arusha) na Catherine Lange (wa Mafunzo).

Washindi hao walizawadiwa fedha taslimu na medali za Dhahabu, Fedha na Shaba kwa kategori zote za wanaume na wanawake, huku washiriki wengine wote kuanzia nafasi ya 10 na kuendelea wakiambulia medali tupu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles