Na Derick Milton, Simiyu
Wakatii ngoma za utamaduni (MBINA) ambazo ufanyika kipindi cha mavuno kama utamaduni wa kabila la wasukuma na kuongoza wanaume tu kila mwaka, upande wa wanawake nao wameandaa ngoma hizo.
Ngoma hizo ambazo hukusanya umati mkubwa wa wananchi, zinatarajia kufanyika Julai Jumatano 7, 2021 siku ya Sabasaba katika viwanja vya CCM Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Kwa mara ya kwanza baada ya kupita muda mrefu, ngoma hizo zitaongozwa na wanawake, ambapo Ofisi ya Mbunge jimbo la Bariadi chini ya Mbunge wake Andrew Kundo imeandaa tamasha hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumanne Julai 6, 2021, Katibu wa Mbunge, Emmanuel Mabula amesema kuwa lengo la mbunge kuanzisha ngoma hizo za wanawake ni kutaka kuhamasisha jamii hasa vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa usahihi kiuchumi zaidi.
“Kauli mbiu ya ngoma hizi ni mbina ya wanawake na matumizi sahihi ya mitandao, lengo la Mheshimiwa mbunge ni kutaka vijana wamuunge mkono Rais Samia Suruhu Hassan kuinua uchumi wan chi kupitia mitandao ya kijamii au kukua kwa teknologia,” amesema Emmanuel.
Aidha ameongeza kuwa katika tamasha hilo la ngoma, makundi mawili kutoka kwenye kabila hilo WAGIKA na WAGALU wanawake watashindana, huku kiasi cha zaidi ya Sh Milioni nne kikishindaniwa kama zawadi kwa mshindi.
Mtaribu wa tamasha hilo, Samwel Bomani amesema kuwa ngoma za asili zinazoongozwa na wanawake zilipotea kwa muda mrefu, ambapo alimpongeza Mbunge huyo kwa ubunifu wake wa kuzirudisha.
Amesema kuwa ngoma hizo zimekuwa muhimu kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu, kwani zinadumisha mila na desturi za kabila hilo, ambapo ametaka wananchi wa mkoa huo kufika katika viwanja hivyo kuona uwezo wa wanawake.
Naye kiongozi upande wa WAGALU wanawake Landu Hamis ametamba kushinda kwenye ngoma hizo, huku akimtisha mwenzake Mgika kuwa atampoteza na kumbeba juu ya fisi mchana.
Debora John wa WAGIKA amesema kuwa uwezo wake ni mkubwa na hawezi kushindwa na Wagalu kuwa atamchukua kwenye kimbunga na ungo na kumpoteza kusikojulikana.