29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Naibu Waziri Utalii mgeni rasmi kongamano la Utalii Mwanza

Na Clara Matimo,Mwanza

Mamia ya Vijana kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanatarajia kukutana kesho Alhamis Juni 24,2021 jijini Mwanza kwenye kongamano la uwekezaji katika sekta ya utali ili wazijue fursa zilizopo waweze kujiajiri.

Kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, Mratibu wa Kongamano hilo kutoka Taasisi ya Tamaduni Intertainment and production, Abdallah Ramadhani, amesema wameamua kuandaa kongamano hilo baada ya kufanya utafiti na kubaini kwamba vijana wengi waliohitimu kozi mbalimbali katika sekta ya utalii hawana ajira.

“Sisi tunaziona fursa nyingi katika sekta ya utalii lakini wapo baadhi ya vijana wenzetu wamehitimu kozi mbalimbali katika sekta ya utalii kila siku wanailalamikia serikali kwamba haiwaajiri, tukaona tunaweza kukutana kupitia kongamano la siku mbili tuliloliandaa kuanzia Juni 24 na 25 ili kuhamasishana kuzitumia fursa za kibiashara ambazo tumeziona nao wazitumie kujiajiri.

“Hakuna haja ya kuilaumu Serikali kuhusu ajira, jamani vijana wenzetu watambue kwamba miaka ya nyuma wahitmu wa kozi za utalii walikuwa wachache na uhitaji wa rasilimali watu ulikuwa mkubwa lakini siku hizi wahitimu ni wengi na vyuo vinavyotoa kozi za utalii ni vingi hivyo ni vigumu wote kuajiriwa lakini kupitia kozi walizosoma elimu waliyonayo wakionyeshwa fursa zilizopo watajiajiri.

“Hata ambao hawajasoma kozi za utalii wakihudhuria kongamano hili hakika kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wadau wa utalii wataona fursa maana zipo nyingi sana, nawasihi vijana wenzangu kutoka mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa jirani wasikose,” amesema Ramadhani.

Naye Mkuu wa Hifadhi Kisiwa cha Saanane, Eva Mallya, amesema watatoa mada mbalimbali katika kongamano hilo ambazo zitawaonyesha vijana fursa za utalii zilizopo na vivutio ambavyo vipo katika hifadhi za taifa ziwachagize kujiajiri kupitia sekta hiyo.

“Kuna aina nyingi za utalii bado hazijatumiwa vizuri, yapo maeneo ya utalii ambayo siyo lazima mtu atoke akawekeze. zipo shughuli ambazo mtu anaweza akabuni zikafanyikia ndani ya hifadhi ya taifa na mbunifu huyo akafaidika yeye  pamoja na Serikali, hivyo nichukue fursa hii kuwasihi vijana wa mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa jirani waje tuungane kesho na kesho kutwa hapa jijini Mwanza Rock City Mall tupeane elimu jinsi ya kufanya biashara katika sekta ya utalii,”alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Tamaduni intertainment and production Wambura Mwikwabe, katika kongamano hilo wajasiriamali watapata fursa ya kuonyesha  bidhaaa mbalimbali za utalii.

“Kongamano hili litakuwa endelevu, kila mwaka tutakuwa tunafanya ili vijana waendelee kupata mafunzo na pia ambao wameishanufaika watakuwa wanakuja kwa ajili ya kuwahamasisha wenzao,  taasisi yetu inajishughulisha na  mambo ya utamaduni kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho hivyo tutawakutanisha vijana na taasisi za kifedha zinazoweza kuwawezesha kuwekeza katika biashara ya utalii kwa ufanisi,” alisema Mwikwabe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles